
*****************************
Na JUMA ISSIHAKA
NAIBU Waziri wa
Viwanda na Biashara Mhandisi Stella Manyanya, amewataka wawekezaji
nchini kufuatilia sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji ili kuepuka
ukiukwaji wa sheria na
kusababisha ukinzani na taasisi za udhibiti za
serikali.
Hayo aliyasema
wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya viwanda na Biashara mkoani Pwani
ikiwa ni mara ya pili mfululizo kwa maonyesho hayo kufanyika mkoani
humo.
Alisema kwa muda
mrefu kumekuwa na changamoto za migogoro baina ya taasisi za udhibiti na
wamiliki wa viwanda ambazo zinatokana na uelewa mdogo wa kanuni za
uendeshwaji wa viwanda nchini.
“Wenye Viwanda
wajibikeni kuhakikisha mnatambua taratibu za kisheria za uendeshaji na
uanzishaji wa viwanda ili kupunguza migongano na taasisi za udhibiti,
tunatambua kuwa wakati mwingine taasisi hizi nazo zinakuwa na matatizo
hivyo tunafanya kila namna kukabili,” alisema.
Alizitaka taasisi
za udhibiti kutowatoza faini wamiliki wa viwanda pasi na kuwapa maelezo
ya kutosha kuhusu makosa yanayopelekea kutozwa faini hizo.
Mhandisi
Manyanya, aliongeza kuwa maonyesho hayo yakatumike kama chachu ya
kuvutia wawekezaji wengine kutokana na kukua kwa soko la bidhaa za
viwanda nchini.
BRELA
Akizungumza
katika maonyesho hayo Msajili Mwandamizi wa Viwanda, Wakala wa Usajili
wa Biashara na Leseni (BRELA) Yusuph Nakapala, alisema ushiriki wao
katika maonyesho hayo ni kuhamasisha jamii kusajili kampuni na bidhaa
zao.
Alisema kwa sasa
BRELA imewawezesha mfumo wa kusajili kampuni na biashara zao kwa njia ya
mtandao kwa shabaha ya kuwapunguzia gharama na usumbufu wamiliki.
“Sisi tupo hapa
kutoa elimu kwa jamii juu ya kusajili kampuni zao na kama inavyojulikana
kwamba kwa sasa tunafanikisha hilo kwa njia ya mtandao hivyo
tunatarajia wenye viwanda wengi watatembelea banda la BRELA,” alisema.
Aliongeza kwa
kuzitaka kampuni zilizopewa siku 90 kukamilisha usajili kwa njia ya
mtandao kufanya hivyo ndani ya muda huo na kwamba maonyesho hayo ndiyo
fursa kubwa ya kupata elimu ya usajili kwa mfumo huo.
BRELA ilianza
mfumo wa usajili kwa njia ya mtandano tangu Januari mosi mwaka jana na
sasa ipo katika majaribio ya mfumo wa usajili wa leseni ya biashara
daraja A.
No comments :
Post a Comment