Muonekano wa Kivuko kipya cha
Kayenze Bezi ambacho ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba
mwaka huu, kivuko hicho kimegharimu jumla ya shilingi Bilioni 2.7 za
Kitanzania na kitatoa huduma kati ya Kayenze na Bezi Wilaya ya Ilemela
mkoa wa Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akitoa taarifa fupi wakati
wa ziara ya Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TEMESA Profesa Idriss
Mshoro kulia ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko viwili vipya vya
Chato Mharamba na Bugorola Ukara vinavyogharimu jumla ya shilingi
bilioni 7.3 za Kitanzania. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. John
Mongella.
Meneja wa Kampuni ya Songoro Major
Songoro (wa pili kushoto) akimpa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza
Mhe. John Mongella katikati wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya
ujenzi wa vivuko viwili vipya vya Chato Mharamba na Bugorola Ukara
vinavyogharimu jumla ya shilingi bilioni 7.3. Wa kwanza kulia ni
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y.
Maselle na Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TEMESA Profesa Idrissa
Mshoro.
Meneja wa Kampuni ya Songoro Major
Songoro kulia akimpa maelezo kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza Mh. John
Mongella wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko viwili
vipya vya Chato Mharamba na Bugorola Ukara vinavyogharimu jumla ya
shilingi bilioni 7.3 za Kitanzania.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA)
……………………
NA ALFRED MGWENO- TEMESA MWANZA
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA) inatarajiwa kukamilisha ujenzi wa
vivuko viwili vipya
vinavyogharimu jumla ya shilingi bilioni 7.3 ifikapo mwezi Februari
mwaka 2020.
Hayo yamebainishwa leo na Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle
wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala huo Profesa
Idrissa B. Mshoro alipotembelea yadi ya Songoro Ilemela jijini Mwanza
kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko hivyo unaoendelea katika karakana
hiyo ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella alialikwa
kushuhudia ukaguzi huo.
Mhandisi Maselle alisema mkataba
kwa ajili ya ujenzi wa kivuko cha Bugorola Ukara ulisainiwa Tarehe 8
mwezi Februari mwaka huu wakati ule wa Chato Mharamba ulisainiwa Tarehe
15 mwezi Aprili na ujenzi wa vivuko vyote unafanywa na kampuni hiyo ya
kizalendo ya Songoro Marine.
‘’Ujenzi wa kivuko cha Bugorola
una gharama ya shilingi za Kitanzania bilioni 4.2 wakati ule wa Chato
Nkome ni wa shilingi bilioni 3.1 bila VAT na fedha zote hizi zinatolewa
na serikali ya Tanzania.’’ Alisema Mtendaji Mkuu.
Aliongeza kuwa Wakala unaendelea
na ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV. Sengerema kwa gharama ya shilingi
milioni 689.4 na utakamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu huku ule wa
kivuko cha Kayenze Bezi unaogharimu bilioni 2.7 ukitarajiwa kukamilika
ifikapo mwezi Novemba.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala
huo Profesa Idrissa B. Mshoro akizungumza katika ziara hiyo alisema
ununuzi wa vivuko hivyo ni jitihada za serikali katika kuboresha huduma
kwa wananchi na kuhakikisha maeneo mengi ya nchi yanafikika kirahisi ili
kuinua uchumi wa nchi hasa katika kulenga kufikia malengo ya nchi ya
uchumi wa kati kufikia 2025.
‘’Naomba niishukuru serikali tena
kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vivuko hivi ambavyo vitakuwa ni
mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo kwani vitawaondolea adha ya usafiri
waliyonayo kwa sasa hasa wananchi wenye kipato cha chini na mimi na
bodi yangu tutahakikisha tunaisimamia vizuri TEMESA ili kutimiza malengo
hayo.’’ Alisema Profesa Mshoro.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.
John Mongella akizungumza katika ziara hiyo aliishukuru serikali kwa
kuendelea kurahisisha usafiri wa vivuko katika mkoa huo ambapo vivuko
vyote vikikamilika vitafanya idadi ya vivuko katika mkoa huo kutoka 11
na kufikia 14 ikiwemo boti moja ya uokozi ya (SAR II).
‘’Nichukue fursa hii kuwapongeza
TEMESA kwa usimamizi mzuri na kazi nzuri wanayoifanya katika kuboresha
miundombinu ya vivuko kote nchini.’’ Alisema Mhe. Mongella.
Kukamilika kwa miradi hii mipya ya
vivuko kutaifanya TEMESA kutoka kuwa na vivuko 30 na kufikia kuwa na
jumla ya vivuko 34 nchi nzima.
No comments :
Post a Comment