Tuesday, October 29, 2019

UZINDUZI WA VITAMBULISHO VIPYA VYA KIELEKTRONIKI (SMART CARDS) VYA MZANZIBAR MKAAZI



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiangalia mfano wa Kitambulisho chake kipya cha Kielektroniki (SMART CARDS) cha Mzanzibar Mkaazi wakati wa  Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar chini ya usimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar,[Picha na Ikulu]   29/10/2019.
Baadhi ya Wananchi wa waliohudhuria katika ya Uzinduzi rasmi wa  Vitambulisho vipya vya Kielektroniki (SMART CARDS) vya Mzanzibar Mkaazi uliofanywa na  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (hayupo pichani)  katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar chini ya usimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar,[Picha na Ikulu]   29/10/2019.
Mke wa Rais wa Zanzibar  Mama Mwanamwema Shein akionesha kitambulisho chake  kipya cha Kielektriniki (SMART CARDS) mara baada ya kukabidhiwa  na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(hayupo pichani)   wakati wa Uzinduzi rasmi wa Vitambulisho hivyo uliofanyika leo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu] 29 /10/2019.
***************************************
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein amesema matumizi ya Vitambulisho vipya vya Mzanzibari
mkaazi (smart card) yataiwezesha serikali kuweka na kuhifadhi
kumbukumbu za matukio ya watu wote katika Daftari la Usajili na
Utambuzi.
Dk. Shein amesema hayo katika uzinduzi wa Kadi mpya za Kielektronik ya
Mzanzibari mkaazi, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul
wakil Kikwajuni mjini hapa.
Alisema matumizi ya vitambulisho hivyo vitaisaida Serikali, taasisi na watu
binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbali mbali zenye
mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.
Aidha, alisema kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya
utaisadia serikali katika kuwatambuwa watu wanaostahiki kupata haki za
msingi , kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.
“Itawezesha kumtambua mtu anaestahiki kupata haki yake kama vile
malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na
nyenginezo”, alisema.
Dk. Shein alisema kutokana na vitambulisho hivyo Serikali itapata urahisi
katika suala zima la ukusanyaji wa mapato hivyo kuimarisha huduma
muhimu za kijamii, ikiwemo afya, elimu, barabara pamoja na ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
Alisema kimsingi Serikali inapaswa kuwa na nyenzo katika udhibiti wa
amani na utulivu wa watu wake, hivyo ni dhahiri Vitambulisho vipya vitakavyotumika hivi sasa ni vyenye ubora wa hali ya juu na uwezo wa
kuhifadhi taarifa nyingi za mtumiaji.
Alieleza kuwa vitambulisho hivyo vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo
sio rahisi kughushiwa, vikiwa na uwezo mkubwa wa kiusalama wa taarifa
za mtumiaji, akibainisha kutumika katika nchi kadhaa duniani.
Rais Dk. Shein alitowa wito kwa wakaazi wote wa Zanzibar waliofikia umri
wa miaka 18 kwenda kujisajili katika ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio
ya Kijamii zilizopo katika Wilaya zote nchini, sambamba na wale ambao
bado hawajajiandikisha kufanya hivyo.
Aidha, aliwataka watendaji wanaohusika na utayarishaji wa vitambulisho
hivyo, kuwa makini na waangalifu katika utoaji wake.
Vile vile aliwataka Wakuu wa Mikoa kusimamia vizuri taarifa za uhakiki wa
watu walioko katika maeneo yao, kuanzia ngazi za shehiya, wadi na Wilaya
ili kuhakikisha wanawatambua wananchi wao na taarifa zao zilizo sahihi.
“Ni muhimu mlifanyie mapitio daftari la wakaazi katika shehiya, ambalo
ndio msingi wa uthibitisho wa kujua taarifa za utambuzi na makazi ya watu
waliomo katika maeneo yenu”, alisema.
Dk. Shein aliwataka wananchi kutambua jukumu la kuisadia Ofisi ya
Wakala wa Usajili wa matukio ya kijamii katika kutambuwa wakaazi wa
maeneo yao badala ya kuiachia jukumu hilo Ofisi hiyo pekee.
Aidha, aliwataka wananchi kuondokana na tabia ya kutumia njia za mkato
katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, akibainisha hatua hiyo imekuwa
chanzo cha kuibuwa rushwa.
“Naendelea kukunasihini watendaji wote wa Wakala wa Usajili wa matukio
ya kijamii Zanzibar, mfanye kazi zenu kwa uadilifu, uzalendo na
mfungamane na misingi ya haki na sheria pamoja na kufuata taaribu
zilizowekwa katika kuendesha Ofisi ”, alisema.
Alisisitiza haja ya kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini,
akibainisha kuwa ni hazina isiyopaswa kuvurugwa na kusema bila ya
kuwepo amani na utulivu nchini, hakutakuwa na meendeleo yoyote
yatakayofikiwa,
Alisema kukamilika kwa mradi huo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji
wa Ilani ay Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015-
2020, inayolenga kuwapatia huduma bora wananchi.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi umuhimu wa
kutembea na Kadi ya Utambulisho wa Mzanaiabari mkaazi mahala popote
ndani ya nchi, akibainisha faida kubwa ya jambo hilo.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa
na Idara maalum za SMZ, Haji Omar Kheir aliwataka wananchi wote wenye
sifa za kisheria kufika katika vituo vya usajili vilivyopo kila Wilaya nchini.
Alisema vitambulisho vipya vya Mzanzibar mkaazi ndicho kitakachotumika
katika upatikanaji wa huduma mbali mbali muhimu kama vile upatikanaji wa
leseni, miamala ya fedha, mahitaji katika taasisi za umma pamoja na zile
zenye mahitaji ya vitambulisho.
Aidha, alisema Wizara hiyo itaendelea kusimamia utoaji wa elimu kwa
wananchi ili kutii sheria ya ukaazi na kupata fursa mbali mbali ziliopo
nchini.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili na matukio ya kijamii
Zanzibar, Dk. Hussein Khamis Shaaban alisema Ofisi hiyo itaendelea na
mikakati ya kusajili na kuwapatia vitambulisho wananchi wote wenye sifa
za kisheria.
Alisema mfumo wa vitambulisho vya kielektronic ni ufunguo katika kufikia
maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kudumisha ulinzi na
usalama katika nchi.
Aidha, alisema Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa ya uingiaji wa
wageni kutoka nje, hivyo kuwepo kwa vitambulisho hivyo ni muhimu kwani
kutawezesha kuwatambuwa wageni hao.
Katika hafla hiyo, pamoja na mambo mengine, Dk. Shein alipata fursa ya
kutembelea Ofisi za Wakala wa Usajili wa matukio ya Kijamii Zanzibar
ziliopo Mazizini na kuangalia vifaa mbali mbali vinavyotumika kutayarishia
vitambulisho hivyo.
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na
Idara maalum za SMZ Haji Omar Kheri alimkabidhi Dk. Shein Kitambulisho
kipya cha Mzanzibari mkaazi , ambapo nae alipata fursa ya kuwakabidhi viongozi mbali mbali wa serikali , akiwemo Mama Mwanamwema Shein pamoja na Wananchi kadhaa.

No comments :

Post a Comment