Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Dkt Edwin Mhede akizungumza na Waandishi wa habari mkoani Mbeya leo,kuhusu mamlaka hiyo ilivyokusanya mapato
jumla ya Shilingi Trilioni 1.7 katika kipindi cha mwezi Septemba 2019,
ambayo ni sawa na asilimia 97 ya lengo la mwezi huo ambayo ni Trilioni
1.8 .
Baadhi
ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Dkt Edwin Mhede alipokuwa
akizungumza nao leo mkoani Mbeya kuhusu mamlaka hiyo
ilivyokusanya mapato yake yenye jumla ya Shilingi Trilioni 1.7 katika
kipindi cha mwezi Septemba 2019, ambayo ni sawa na asilimia 97 ya lengo
la mwezi huo ambayo ni Trilioni 1.8 .
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya mapato ya Serikali jumla ya TZS
1.767 trilioni katika kipindi cha mwezi Septemba 2019. Makusanyo haya,
ambayo ni sawa na ufanisi wa 97.20% ya lengo letu la kukusanya jumla ya
kiasi cha TZS 1.817 trilioni katika kipindi cha mwezi Septemba 2019,
hayajawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa TRA. Kwa kulinganisha na
makusanyo ya mwezi Septemba 2018, makusanyo haya ya mwezi Septemba 2019
yamekua kwa wastani wa 29.18%.
Ufanisi
huu wa mwezi Septemba 2019 ni mwendelezo wa ongezeko la makusanyo tangu
mwaka wa fedha wa 2019/2020 ulipoaza mnamo mwezi Julai 2019. Hii ni kwa
sababu katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2019, TRA tulifanikiwa
kukusanya kiasi cha TZS 1.256 trilioni (ambayo ilikuwa ni ufanisi wa
91.92% ya lengo la kukusanya TZS 1.367 trilioni) na TZS 1.335 trilioni
(sawa na ufanisi wa 96.05% ya lengo la kukusanya TZS 1.409 trilioni),
sawia. Aidha, makusanyo haya ni kiashiria kwamba Walipakodi na
Watanzania walio wengi sasa wameelewa, wamekubali, na wameitikia wito wa
Serikali ya Awamu ya Tano wa kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya
maendeleo ya Taifa letu.
Hivyo,
TRA inawashukuru walipakodi wote waliochangia makusanyo hayo kwa kulipa
kodi zao kwa hiari. Pia, tunaishukuru Serikali (kwa ujumla wake) kwa
kuendelea kuisaidia TRA katika kutekeleza majukumu yake ya kukusanya na
kuhasibu mapato ya Serikali.
Kwa
namna ya kipekee, tunapenda kuvishukuru vyombo vya habari kwa juhudi
wanazofanya kuwahabarisha na kuelimisha umma juu ya ulipaji kodi. Aidha,
tunapenda kuwahimiza wale wote ambao bado wanasuasua kujitokeza kulipa
kodi hizo kwa wakati. Vile vile, tunaendelea kuwasisitiza walipakodi na
wananchi wote ambao wana changamoto za kikodi kutembelea Ofisi za TRA na
kuonana na Makamishna, Mameneja wa Mikoa, na Mameneja wa Wilaya kwa
ufumbuzi wa changamoto hizo.
Pamoja
na mafanikio haya, tunajua kuwa bado hatujafikia malengo yetu. Aidha,
TRA tunatambua kuwa mafanikio haya yanakuja na changamoto. Ni lazima
sote, kwa maana ya walipa kodi na Watendaji wa TRA, tukabiliane na
changamoto hiyo na tuishinde. Kwa pamoja tunaweza kuishinda changamoto
hiyo ambayo ni kuhakikisha uendelevu wa ufanisi huu mkubwa kwa miezi
ijayo. Hivyo, nawatia moyo walipa kodi na Watumishi wenzangu kuwa bado
tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na
kuzidi.
Baadhi
ya mikakati iliyopelekea kiasi hiki kikubwa cha ukusanyaji ni pamoja na
kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kusimamia kikamilifu Sheria za kodi,
kuweka msisitizo wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za
kielektroniki (EFD receipts), elimu kwa mlipakodi, kuendelea kukujenga
mifumo rafiki ya ukusanyaji kodi, na zoezi linaoendelea la kuboresha
huduma kwa mlipakodi.
Wakati
huo huo, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wamiliki wote wa majengo nchini
kujitokeza kulipia kodi za majengo haraka iwezekanavyo. Hii itawaepusha
na usumbufu wa kulipa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwani kwa
sasa viwango ni rafiki na vinalipika. Viwango hivyo kwa mwaka ni TZS
10,000 kwa nyumba ya kawaida, TZS 50,000 kwa kila sakafu nyumba ya
ghorofa katika Majiji, Manispaa, na Halmashauri za Miji, na TZS 20,000
kwa jengo la ghorofa katika maeneo ya Halmashauri za Wilaya. Wamiliki
wote wa majengo mnaweza kulipa kodi hii kwa njia ya simu za mkononi.
Halikadhalika, Mameneja wa TRA katika Ofisi zetu za Mikoa na Wilaya
wameweka utaratibu mzuri wa kumwezesha kila Mmiliki wa jengo kulipa kodi
ya majengo kwa wakati.
Katika
hatua nyingine, TRA inawaasa wale wote wanaojishughulisha na vitendo
viovu vya kughushi risiti za kielektroniki za EFD. Tunatoa onyo kwamba
muache mara moja tabia hiyo. Hii ni kwa sababu, kwa oparesheni
tunayoendelea nayo ya kufuatilia matumizi sahihi ya EFD, kwa
wataobainika watachukuliwa hatua kali za Kisheria ikiwa ni pamoja na
kufikishwa mahakamani. Kila mwananchi na mfanyabiashara atambue wajibu
wake uliopo kwa mujibu wa Sheria wa kudai risiti kwa kila manunuzi na
kutoa risiti kwa kila mauzo.
Kwa
sasa TRA imesogeza huduma karibu na walipakodi na wananchi kwa ujumla
kwa kuwa sasa mnaweza kupiga simu bure kupitia namba 0800750075 au
0800780078 na kwa upande wa barua pepe tafadhali tuandikie huduma@tra.go.tz. Vile vile, mnaweza kutuma ujumbe kupita namba ya Whatsapp +255744233333.
Tunatanguliza shukrani zetu kwa ushirikiano mnaoendelea kuipatia TRA katika kutekeleza majukumu yetu.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na:
Dr. Edwin P. Mhede, Ph.D.
KAMISHNA MKUU
No comments :
Post a Comment