Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi,
Kangi Lugola, akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi makazi
ya Katumba, Mkoani Katavi, leo, ambao amewakatalia raia wa makazi ya
Katumba, Ulyankulu na Mishamo kushiriiki uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa kuwa maombi yao bado
yanafanyiwa kazi.
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi,
Kangi Lugola (kushoto), akimsikiliza Mkazi wa Kijiji cha Ndui Station,
Kata ya Katumba, Mkoani Katavi, Zephania Mshinga (84) wakati alipokuwa
anatoa historia yake alivyokimbia vita Burundi mwaka 1972, na kuingia
nchini kwa ajili ya kuokoa maisha yake. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………
Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI wa Mambo ya ndani ya Nchi,
Kangi Lugola, amesema wananchi waliopewa uraia katika Makazi ya
Wakimbizi ya Katumba, Ulyankulu na Mishamo nchini hawatashiriki
kugombea
na kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa
kufanyika hivi karibuni, kwa kuwa maombi yao bado yanafanyiwa kazi.
Akijibu maombi ya raia hao
waliopo Kata ya Katumba, Mkoani Katavi, Waziri Lugola alisema maombi yao
wanayo na Serikali inayafanyia kazi kwa ukaribu zaidi, hivyo wanapaswa
kuwa wavumilivu kusubiri majibu yao.
“Serikali inawajali,
inawathamini, na pia maombi yenu tunayo, na tunayafanyia kazi kwa
ukaribu zaidi kwa kuwa Serikali ya Rais Dkt. Magufuli ni sikivu, naomba
muendelee kusubiri bila kuwa na uharaka wowote,” alisema Lugola.
Akisoma hotuba ya wananchi hao
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ndui Station, Diwani wa
Kata hiyo, Seneta Baraka alisema wananchi hao wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo kutopata haki ya kushiriki uchaguzi wa
serikali za mitaa mwaka huu 2019.
“Ombi letu kwako mheshimiwa
Waziri ni kuturuhusu kufanya uchaguzi katika mazingira haya sawa na
ilivyofanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ikiwa haiwezekani basi ombi
letu na changamoto zitatuliwe na tupewe fursa ya kufanya uchaguzi mara
baada ya changamoto hizo kutatuliwa,” alisema Baraka.
Baraka alisema raia hao
walimuomba Waziri huyo, kubalidilisha hadhi ya eneo la Katumba, Mishamo
Mkoani Katavi, na Ulyankulu Mkoani Tabora, kuwa na hadhi ya Serikali ya
Mitaa kwa kuwa hadhi ya makazi ya wakimbizi inawanyima fursa nyingi za
kimaendeleo.
Maombi mengine waliyoyatoa kwa
Waziri huyo ni kukamilisha mchakato wa uraia kwa vijana wao uliofanyika
mwaka 2017, wakidai kuwa Serikali ilikamilisha mchakato wa uraia wa
awamu ya kwanza uliofanyika mwaka 2007, wapo ambao maombi yao
hayajakamilika hadi sasa.
Pia waliomba usajili wa laini za
simu kwa wenzao ambao hawajakamilisha mchakato wa uraia ili waweze
kupata vitambulisho vya taifa.
Akijibu changamoto hizo, Waziri
Lugola aliwaambia raia hao maombi hayo yapo mezani kwake na Serikali
inayafanyia kazi kwa ukaribu na watapewa majibu mara watakapomaliza
kuyafanyia kazi.
Kwa ombi la usajili wa laini za
simu, Lugola alisema hiyo ni haki yao kupata vitambulisho, nakuwaahidi
kuwa suala hilo litashughuliwa kwa kuwa zoezi hilo ni endelevu.
Kwa upande wake, Mkazi wa Kata
hiyo ambaye alikimbia vita mwaka 1972 akitokea nchini Burundi, Zephania
Mshinga ambaye ana umri wa miaka 84, alisema Tanzania ni nchi salama, na
pia hayupo tayari kuiacha nchi hiyo ambayo ina amani, utulivu, na watu
wakarimu.
“Msiombee vita jamani, nilifika
hapa Tanzania mwaka 1972 wakati Burundi kulipokuwa na vita, nashukuru
nimepewa uraia na kama nikinyang’anywa uraia huu sina mahali pa kwenda,
siwezi kurudi nilipotoka maana miaka mingi imepita, sasa ni mkazi wa
hapa, naishukuru Serikali ya Tanzania,” alisema Mshinga.
Waziri Lugola yupo Mkoani Katavi
kwa ziara ya siku tano ya kikazi, akikagua miradi ya maendeleo,
kuzungumza na askari na watumishi wa Wizara yake, pamoja na kusikiliza
kero za wananchi katika mikutano ya hadhara mkoani humo
No comments :
Post a Comment