Sunday, September 29, 2019

Serikali yavunja Mkataba na Mkandarasi Ujenzi wa Jengo la Polisi Manyara

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul akiongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kushoto),baada ya kumaliza Kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Manyara juu ya Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Jeshi la Polisi mkoani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (meza kuu) akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Polisi  baada ya kuwasili leo kwa ziara ya kikazi huku akitoa taarifa ya Serikali kuvunja Mkataba na Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi la  Polisi mkoani Manyara  lengo ni kuepuka gharama za ujenzi huo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (meza kuu) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Manyara baada ya kuwasili leo kwa ziara ya kikazi huku akitoa taarifa ya Serikali kuvunja Mkataba na Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi la  Polisi mkoani hapo lengo ni kuepuka gharama za ujenzi huo.Wa kwanza kulia ni Mbunge wa Babati Mjini,Pauline Gekul.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
**********************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali imewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Manyara kuanza na kumalizika kwa
Mradi  Ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi  ambao ulisimama tangu mwaka 2012 kutokana na gharama kubwa ya ukandarasi na sasa utajengwa kwa kutumia utaratibu mpya wa serikali wa nguvu mali ambao utapunguza gharama za ujenzi kulinganisha na kutumia mkandarasi
 Hayo yamesemwa leo  na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni alipotembelea mradi huo uliopo katika eneo la Komoto Kata ya Bagara Wilayani Babati Mkoani Manyara ambao gharama za awali za mradi huo ni  Milioni Mia Tano Themanini na Moja,Laki tatu na Thelathini.
“Serikali tunawahakikishia wananchi wa Mkoa wa Manyara kujengwa kwa jingo la polisi ili masuala ya ulinzi na usalama yaweze kuwa imara katika mkoa huu,tayari timu maalumu kutoka makao makuu ya polisi ilishafika hapa na kuona jinsi mradi huu utakavyoweza kuendelea baada ya kusimama kwa takribani miaka saba sasa,” alisema Naibu Waziri Masauni
“Juhudi mbalimbali zishaanza na hivi navyozungumza tayari Jeshi la polisi mkoani hapa likishirikiana na wadau wameshafanya harambee na kufanikiwa  kukusanya  takribani  kiasi cha Shilingi Milioni Arobaini na Tano na sisi kama Wizara tutachangia ujenzi huo” aliongeza Masauni
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo la mradi Mbunge wa Babati Mjini Pauline Gekul alisema Jeshi la Polisi linafanya kazi katika mazingira madogo,ofisi ni ndogo hali inayopelekea huduma kutolewa kwa uchache tofauti na mahitaji
“Nashukuru kuona serikali leo imefika kuona maendeleo ya huu mradi kwa kweli polisi wanahitaji jingo jipya ili kazi ya kulinda amani na utulivu iwe rahisi kwao,tunashukuru pia wadau mbalimbali wameanza kutuunga mkono ikiwa pia na ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya askari wetu” alisema Mbunge  Gekul
Awali akitoa taarifa ya Uhalifu Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Cyprian Mushi alikiri kupungua  kwa uhalifu huku akikiri kuwepo changamoto katika kutatua baadhi ya kesi za ubakaji baada ya familia za mtuhumiwa na familia ya mtuhumu kutotokea mahakamani baada ya kuzimaliza kesi hizo kifamilia.

No comments :

Post a Comment