Na Veronica Simba – Dar es Salaam
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amesema pamoja na kwamba Tanzania
imeshagundua gesi futi za ujazo trilioni 57.54 hadi sasa, bado inahitaji
gesi zaidi
itakayosaidia kuimarisha uchumi wa viwanda.
itakayosaidia kuimarisha uchumi wa viwanda.
Aliyasema
hayo jana Agosti 3, 2019 jijini Dar es Salaam, alipokutana na
kuzungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC).
Alisema,
kazi ya utafutaji wa gesi inaendelea vizuri lakini akaisisitiza
Menejimenti hiyo kuongeza kasi zaidi katika utafutaji wake pamoja na wa
mafuta.
“Mahitaji
ya gesi ni makubwa. Tunahitaji gesi kuzalisha umeme, tunahitaji gesi ya
kutosha kwa matumizi ya majumbani na pia viwandani,” alieleza.
Aidha,
Waziri aliitaka Menejimenti husika kutafuta mbinu mbalimbali na
kuongeza ubunifu ili shirika hilo liweze kufanya biashara kiushindani,
lipate mapato na baadaye lianze kutoa gawio serikalini.
Akifafanua,
alisema, mwaka 2015 ilipitishwa sheria mpya ya mafuta ambayo ilibadili
majukumu ya shirika kutoka kutegemea ruzuku ya serikali na kuwa shirika
lenye kujiendesha kibiashara.
“Sasa, TPDC ikiwa ni kampuni ya serikali yenye kufanya biashara, ni lazima ifanye biashara kiushindani.”
Waziri
alilitaka shirika hilo kupanua wigo wa usambazaji gesi majumbani
hususan mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa nishati ya
mkaa, inayosababisha ukatwaji wa miti kwa kiwango kikubwa.
Vilevile,
alitaka viwanda vingi zaidi viunganishiwe mfumo wa gesi kutoka 40
vilivyopelekewa huduma hiyo, ili kuvipunguzia gharama ya uzalishaji
inayotokana na matumizi ya nishati nyingine.
Kwa
upande wa matumizi ya gesi kwenye magari, Dkt Kalemani aliiagiza TPDC
ifungue vituo zaidi vya kujazia gesi katika mikoa mbalimbali ili wateja
walioko mikoani wapate huduma ya kubadili mfumo wa magari yao kutoka ule
unaotumia mafuta na kuweka unaotumia gesi, ili kuwaepushia usumbufu wa
kufuata huduma hiyo Dar es Salaam ambako ndiko kuna kituo pekee kwa
sasa.
Aidha,
alilitaka shirika hilo kuvifufua vituo vyake sita vya mafuta na
kuongeza vingine zaidi ili iendeleze biashara hiyo kama wanavyofanya
PUMA na wengine kwa ajili ya kuongeza mapato yake.
Maagizo
mengine aliyotoa Waziri kwa Menejimenti hiyo ni kuandaa utaratibu wa
kuachana na uagizaji nje ya nchi vifaa mbalimbali vya kusambazia gesi
zikiwemo mita na mabomba, badala yake itumie vile vitakavyozalishwa
nchini.
“Hii
itawezesha viwanda vya aina hiyo kujengwa hapa nchini, watanzania
watapata ajira na pia itarahisisha zoezi la kusambaza gesi maana vifaa
vitakuwa vikipatikana nchini.”
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Dkt. James Mataragio,
alimhakikishia Waziri kuwa shirika lake litatekeleza kikamilifu maagizo
yote aliyowapatia.
“Tayari
tumeshaanza kujipanga katika maeneo yetu ya kazi yanayojumuisha
utafiti, uzalishaji na biashara ya gesi. Nimerudi nikiwa na nguvu mpya
kuwatumikia watanzania,” alisema Dkt Mataragio ambaye amerudishwa katika
nafasi hiyo na Rais John Magufuli hivi karibuni, baada ya kusimamishwa
kwa muda.
Kikao
hicho pia kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara akiwemo Katibu
Mkuu, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,
Raphael Nombo pamoja na Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi Adam Zuberi.

No comments :
Post a Comment