Rais Dkt. John Pombe Magufuli
akihutubia Mkutano wa Sita Jukwaa la Uongozi la Afrika katika Ukumbi wa
Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam, Tanzania.
*************
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Rais John Magufuli wa Tanzania
amesema masalia ya fikra za kikoloni walizonazo Waafrika wengi ni
miongoni mwa sababu zinazofanya Bara la Afrika kushindwa kusimamia
rasilimali
zake ili kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Ameyasema hayo jijini Dar es
Salaam alipokuwa akihutubia kongamano la viongozi la 2019 akisema dhana
ya uhuru haiwezi kutenganishwa na kujitegemea.
“Kama hujitegemei huwezi kuwa huru, kwani uhuru wako utakuwa mikononi mwa unayemtegemea.”
“Maana hasa ya kupigania uhuru ni
kurejesha rasilimali zetu na hasa rasilimali zetu, lakini pia kuwa na
uamuzi kamili wa namna ya kuzisimamia na kuzitumia wa kuzitumia ili
kuleta ukombozi wa kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.
Amesema kutokana na kutoelewa
dhana kamili ya uhuru, nchi za Afrika zinadhani watawala wa zamani ndiyo
wenye uwezo wa kusimamia na kusaidia na kuendeleza rasilimali.
Ametaja pia sababu ya kushindwa kusimamia rasilimali na kuleta mageuzi ya kiuchumi, akisema fedha siyo msingi wa rasilimali.
“Fedha ni matokeo ya mwisho kabisa
ya matumizi ya rasilimali zetu na siyo msingi wa maendeleo. Hata hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji
watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Hakutaja pesa, alijua itakuja
tu kama yale tutayatimiza,” amesema.
Ametaja pia ukosefu wa ubunifu na
teknolojia ya viwanda akisema Afrika haitaweza kusimamia na kutumia
rasilimali zake kiuendelevu bila kuwa na viwanda.
Mbali na viwanda, ametaja
kukithiri kwa migogoro na hali tete ya siasa barani Afrika akisema
inasababishwa na mabeberu wanaotaka kuendelea kutumia maliasili za
Afrika kwa manufaa yao.
“Wakati sisi tunapigana wao wanakula na kamwe hawatataka tuwe na amani, kwani migogoro ndiyo mtaji wao,” amesema.
Ameendelea kutaja pia tatizo la
mikataba na makubaliano yanayoingiwa na wawekezaji katika kutumia
rasilimali akisema, “Na hapa nchi yetu imeliwa sana kutokana na mikataba
mibovu na hasa kwenye madini.”
Kuhusu uharibifu wa mazingira,
Rais Magufuli amesema unasababishwa na ukataji hovyo wa msitu kwa ajili
ya nishati ya majumbani kutokana na gharama kubwa za umeme na gesi
asilia.
“Chanzo kingine ni uchafuzi wa
mazingira unaofanywa na mataifa mengine yaliyoendelea na yenye viwanda
vingi, lakini Afrika ndiyo inayoathirika zaidi a machafuko hayo,”
amesema.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa
na Serikali, Rais Magufuli amesema imetungwa sheria ya kulinda utajiri
na rasilimali na maliasili ya 2017 na kupitiwa upya na kurekebisha
mikataba ya uchimbaji na madini isiyo na manufaa kwa Taifa.
“Tumeweka msukumo mkubwa kwenye
ujenzi wa viwanda na ukuzaji wa teknolojia ya viwanda ili mazao
yanayotokana na rasilimali zetu yasindikwe kwanza kabla ya kuuzwa nje,”
amesema
Alitaja pia uanzishwaji wa mradi
wa bwawa la Nyerere utakaozalisha MW 2115 kwenye bonde la mto Rufiji
kama njia ya kutunza mazingira, kudhibiti nidhamu za watumishi wa umma
na kupamba na rushwa na ufisadi.
Wageni maarufu waliohudhuria
mkutano huo walikuwa marais wastaafu kutoka baadhi ya nchi za Afrika
akiwemo Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Olusegun Obasanjo wa Nigeria,
Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa Tanzania
No comments :
Post a Comment