Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa na kamati
ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Gairo akiangalia huku akizungumza
kwenye miti iliyopangwa kwa ajili ya kuchoma mkaa mara baada ya kufanya
ziara katika Hifadhi ya Msitu wa Kumbulu kujionea miti iliyokatwa
kinyume na sheria katika Hifadhi hiyo wilayani Gairo mkoani Morogoro.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizumgumza na
wananchi wa kijiji cha Kumbulu wakati akitatua mgogoro wa ardhi uliodumu
kwa muda wa miaka 10 ambapo aliwataka wananchi waache kuharibu msitu
huo wa hifadhi.
Wananchi wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri
Mkuu
wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe akizungumza na wananchi wa kijiji
cha kabla Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu
kuzungumza na wananchi hao kuhusu mgogori kati ya Wananchi na Msitu wa
Hifadhi ya Kumbulu.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akikabidhiwa
kabrasha na Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe lenye vielelezo
vya mgogoro wa ardhi kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka huu mbele ya wananchi
wa kijiji cha Kumbulu wilayani Gairo mkoani Morogoro.
Miti iliyopangwa tayari kuchomwa. ( Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametatua mgogoro wa
ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 10 kati ya wanakijiji wa Kumbulu na
msitu wa Hifadhi ya Kumbulu unaosimamiwa na Halmashauri ya wilaya ya
Gairo kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)
Mhe.
Kanyasu amesema mgogoro huo wa ardhi ulianza mwaka 2009 baada ya
kijiji hicho kupanga matumizi bora ya ardhi ambapo kutokana na baadhi
ya viongozi wa kijiji hicho kutokuridhia uamuzi huo na kuanza
kuwachochea wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya msitu
huo.
Kufuatia
hali hiyo, Kanyasu ameagiza kamati iliyosheheni wataalam mbalimbali
ambayo ilikwisha undwa na wilaya ya Gairo igawe upya maeneo hayo kwa
kuzingatia idadi ya watu katika kijiji hicho kwa kuongeza eneo la
kilimo kutoka ekari 1,000 hadi ekari 2,314 kwa kulimega eneo la msitu
wa hifadhi wenye ukubwa wa ekari 5,500 hadi 5000 ili eneo hilo litumike
kwa ajili ya kilimo.
Aidha,
Kanyasu ameagiza eneo la malisho lipunguzwe kutoka ekari 1,641 hadi
ekari 1,000 ili ekari 641 iweze kutumika kwa ajili ya kilimo.
Ameyatoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumbulu wilayani Gairo katika mkoa wa Morogoro.
Kutokana
na malalamiko hayo ya wananchi, Kanyasu aliwaeleza wananchi hao kuwa
mpango wa matumizi bora ya ardhi uliofanyika mwaka 2008 ulibainika
kuwa na kasoro kwa vile baadhi ya wananchi walichukua ardhi kubwa na
kuna wengine walichukua na kuiuza na kuna wengine walihamia kijijini
hapo kwa ajili ya kutafuta ardhi.
Akizungumzia
kuhusu ugawaji huo wa ardhi kwa kila kaya, Mhe. Kanyasu amesema
kijiji hicho kina kaya 642 hivyo kila kaya itagawiwa ekari mbili na
hivyo kufanya jumla ya ekari 1,284 kati ya ekari 2,314.
Awali,
mpango huo wa matumizi bora ya ardhi ulitenga eneo la misitu wa
hifadhi ekari 5,500, eneo la kilimo ekari 1,000 pamoja na eneo la
malisho la ukubwa wa ekari 1, 600 lakini bado viongozi wa kijiji hicho
licha ya kushirikishwa katika mpango huo waliendelea kuwahamasisha
wananchi kuvamia misitu huo kwa madai kuwa hawayatambui maamuzi hayo.
Aidha,
Mhe. Kanyasu amesema kwa vile Msitu huo wa Hifadhi unapakana na vijiji
vitatu ni vyema na vijiji viwili mbali na kijiji cha Kumbulu kama navyo
vina uhitaji ya ardhi viwasilishe maombi yao ili kupunguza migogoro.
Katika hatua nyingine, Mhe, Kanyasu amezionya kaya hizo zitakazopata ardhi ziendeleze ardhi hiyo la sivyo zitanyang’anywa.
Pia,
Kanyasu amevionya vikundi vya watu wenye maslahi binafasi ndani ya
kijiji hicho viache tabia ya kuchochea migogoro ya ardhi la sivyo
Serikali haitasita kuvichukulia hatua kali za kisheria.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe Amewataka wananchi
hao kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo wakati itakapokuwa ikitekeleza
majukumu yake ili kila kaya iweze kupata ardhi kwa ajili ya kilimo
‘’Lazima
mpate ardhi ya kilimo lakini ni muhimu pia kutunza miti iliyopo kwa
vile bila miti hakuna kilimo kwa sababu miti inasidia kuleta mvua.
Alisisitiza Mchembe
Naye,
Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amewataka wananchi hao wakati
wakisubili kugawiwa maeneo kwa ajili ya kilimo wajiepushe na ukataji
miti ovyo katika msitu wa Hifadhi ya Kumbulu.
‘’
Kwa wale wanaotaka kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa kwa ajili ya
kuupeleka sokoni ni lazima mfuate sheria, hata ukitaka kuukata miti
uliopo nyumbani kwako lazima uombe kibali kwa mamlaka inayohusika.’’
Alisisitiza Shabiby
No comments :
Post a Comment