Mkurugenzi
wa Kampuni za Mohamed Enterprises Limited, Mohamed Dewji amempongeza
Rais Magufuli kwa mageuzi makubwa kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Dewji ameyasema hayo leo akifungua kiwanda cha kusaga unga wa mahindi na
ngano cha 21st Century Food Packaging kinachomilikiwa na Kampuni za
Mohamed Enterprises Limited chenye uwezo wa kusaga tani 1,540 kwa siku
“Mheshimiwa
Rais tunaamini kwamba wale wasiokuelewa leo watakuelewa baadae na
wasioelewa lengo wataeleweshwa na matokeo ambayo tunaamini hayako mbali
sana kwani mageuzi makubwa chini ya uongozi wako ndiyo yaliyotushawishi
kuendelea kuwekeza nchini kama unavyoshuhudia leo hii,” amesema.
“Binafsi
ninashuhudia kuimarika nidhamu kwa watumishi wa umma, mkazo mkubwa
serikalini, kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, kupungua kwa
rushwa na kushughulikiwa kwa migogoro ya ardhi nchini pia tumeguswa na
namna ulivyoshugulikia matatizo ya wafanyabishara,” amesema.
Aidha
amesema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vikubwa na vya kisasa
kinachojihusisha na uzalishaji wa unga wa ngano na wa mahindi nchini, na
kwamba kampuni ilianza uwekezaji 2005 na ilianza na kiwanda chenye
uwezo mdogo wa kusaga tani 240 kwa siku pamoja na uwezo wa kuhifadhi
tani 20 tu za nafaka.
“Hivi
sasa kiwanda kimeboreshwa kwa kuwekeza kwenye mitambo mikubwa
iliyogharimu jumla ya Sh. bilioni 105 na inatumia teknolojia ya kisasa
zaidi, uwekezaji huu umefanyika chini ya awamu ya tano, leo tunashuhudia
kiwanda cha mahindi chenye uwezo wa kusaga tani 300 kwa siku, kiwanda
cha ngano chenye uwezo wa kusaga tani 1240 kwa siku, mitambo yenye uwezo
wa kupokea tani 600 kwa saa za nafaka na uwezo wa kuhifadhi nafaka hadi
tani elfu 50,” amesema.
No comments :
Post a Comment