Friday, August 2, 2019

MAKOMBORA MAPYA YA 9M729 YA URUSI YANAYOITIA TUMBO JOTO MAREKANI NA WASHIRIKA WAKE


Marekani inatarajiwa kujitoa rasmi katika mkataba wa nyuklia na Urusi, hatua inayozusha hofu kuhusu ushindani wa silaha mpya.


Mkataba huo unaohusu zana za nyuklia za masafa ya katikati (INF) ulisainiwa na rais wa Marekani Ronald Reagan na kiongozi wa iliyokuwa Sovieti Mikhail Gorbachev mnamo 1987. Ulipiga marufuku makombora ya masafa ya kati ya kilomita 500-5,500.
Lakini awali mwaka huu Marekani na Nato ziliishutumu Urusi kwa kukiuka makubaliano hayo kwa kufyetua aina mpya ya kombora, jambo ambalo Moscow inalikana.

Marekani imesema ina ushahidi kuwa Urusi imetuma kombora aina ya 9M729 linalofahamika kwa Nato kama SSC-8. Tuhuma hizi ziliwasilishwa kwa washirika wa Nato wa Marekani ambao wote waliunga mkono madai ya Marekani

Rais Donald Trump mnamo Februari alitangaza kuwa Marekani itajitoa kutoka mkataba huo iwapo Urusi haitotii, na kuweka tarehe ya mwisho kuwa Agosti 2.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na yeye  amesitisha majukumu ya taifa lake katika mkataba huo muda mfupi baadaye.

Wachambuzi wanahofia kwamba kutibuka kwa makubaliano hayo ya kihistoria huenda kukachangia ushindani mpya wa silaha kati ya Marekani, Urusi na China.

"Kutokana na kuvunjika kwa mkataba huo sasa, tutashuhudia utengenezaji na utumiaji wa silaha mpya," Pavel Felgenhauer, mchambuzi wa zana za Urusi ameliambia shirika la habari la AFP. "Urusi tayari ipo tayari."

Mwezi uliopita, Katibu mkuu wa Nato Jens Stoltenberg ameiambia BBC kuwa makombora ya Urusi - ambayo alisema kuwa ni "ukiukaji wa wazi wa mkataba huo" - yana uwezo wa nyuklia, ambayo ni magumu kuyatambua na yanaweza kufika katika miji ya Ulaya katika muda wa dakika.

"Hili ni jambo zito," aliongeza. " Mkataba wa INF umekuwa jiwe la msingi katika udhibiti wa silaha kwa miongo kadhaa, na sasa tunashuhudia kuvunjika kwa mkataba huo ."

Ameongeza kwamba hakujakuwepo "ishara zozote" kuwa Urusi itatii makubaliano hayo na kwamba "ni lazima tujitayarishe kwa ulimwengu usiokuwa na mkataba wa INF na ulio na makombora zaidi ya Urusi".

Stoltenberg pia alisema kuwa uamuzi wowote wa Nato kuhusu namna gani ya kujibu utatolewa baada ya kupita muda huo wa mwisho uliotolewa.

No comments :

Post a Comment