Madaktari,
wauguzi na mafundi sanifu wa moyo wa mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) wa chumba cha Cathlab wakiwa na nyuso za furaha mara baada ya kumaliza kumwekea
mgonjwa kifaa maalum cha
kurekebisha mapigo ya moyo ili yawe sawa
(kwa jina la kitaalamu Pacemaker) ambacho kimewekwa kwa mgonjwa mwenye umri wa
miaka 101 kifaa hicho huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya
asilimi 30 kwa dakika.
Madaktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye
na Khuzeima Khanbai wakiangalia kifaa maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo ili
yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker) ambacho kimewekwa kwa mgonjwa
mwenye umri wa miaka 101 kifaa hicho huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo
yako chini ya asilimi 30 kwa dakika. Tangu kuanza kwa Taasisi hiyo mwaka 2015
hii ni mara ya kwanza kwa mgonjwa mwenye umri huo kuwekewa kifaa hicho.(PICHA NA JKCI)
Na Ales Mbilinyi -JKCI
Kwa mara ya kwanza madaktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamwekea mgonjwa mwenye umri wa miaka 101 kifaa
maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo
ili yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker).
Kifaa hicho kisaidizi cha moyo huwekewa wagonjwa
ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimi 30 kwa dakika.
Akizungumza baada ya kumfanyia upasuaji mdogo
na kumwekea mgonjwa kifaa hicho Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Yona Gandye alisema mara nyingi wanawawekea kifaa hicho wagonjwa wenye umri wa miaka 80 kushuka chini lakini
leo hii wamevunja rekodi na na kuweka
kwa mgonjwa wa umri wa miaka 101.
“Kabla ya kufanya upasuaji tulimfanyia
mgonjwa uchunguzi wa kina na kugundua mfumo wake wa umeme wa moyo unahitilafu na
mapigo ya moyo yapo chini ya asilimia 20 hivyo tumemuwekea kifaa ambacho
kitausaidia moyo kuongeza mapigo yake na mara baada ya kumwekea kifaa hiki mapigo yake ya moyo yako vizuri kati ya
asilimia 60 na 100 kwa dakika”, alisema Dkt. Gandye.
Akizungumza kwa furaha mara baada ya baba
yake kuwekewa kifaa hicho Saimoni Maina alisema matatizo ya baba yake yameanza mwaka mmoja
uliopita na kutibiwa katika hospitali mbalilmbali Mkoani Manyara na Arusha
ambapo waligundua kuwa mapigo yake ya moyo yapo chini hivyo kumpa rufaa kwa ajili ya kutibiwa katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Baba alikuwa akianguka na kupoteza fahamu mara
kwa mara ndipo tukaamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu ili
kufahamu anasumbuliwa na tatizo gani, tunashukuru
sana uwepo wa Taasisi hii kwani baba yetu ameweza kufanyiwa upasuaji na hali
yake inaendelea vizuri kama mnavyomuona”, alisema Maina.
Kwa upande wake Mzee Benedict Maina alisema kabla ya kufanyiwa kwa upasuaji huo alikuwa
akipata maumivu makali sehemu za moyo, kuanguka, kupoteza fahamu na kushindwa
kutembea lakini baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali yake imebadilika na
maumivu kupungua ukilinganisha na ilivyokuwa awali na anaamini siku chache
zijazo atarudi katika hali yake ya kawaida.
No comments :
Post a Comment