Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima
Na Asha Shaban - Mara
Zaidi ya kaya 22,540 zinadaiwa kuwa na ukosfu wa vyoo bora katika
Manispaa ya Musoma mkoani Mara jambo ambalo linafanya kaya hizo
kujisaidia sehemu zisizo rasmi ikiwemo ndani ya Ziwa Victoria.
Kufuatia kuwepo kwa idadi kubwa za kaya kukosa vyoo mkuu wa mkoa wa
mara Adam Malima alitoa agizo la muda wa siku 60 kwa wakazi wote wa mkoa
huo ambao hawana vyoo kujenga vyoo hivyo ili kuepuka maambukizi ya
magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Akizindua kampeni ijulikanayo kama nyumba ni choo kampeni inayolenga
kuhamasisha matumizi ya vyoo katika jamii mjini hapa jana Mkuu wa mkoa
alisema kuwa ni aibu kubwa kwa wakazi wa mkoa huo kushindwa kujenga vyoo
na kuvitumia ipasavyo katika zama hizi na kwamba atakayeshindwa
kutekeleza agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mbali na kutoa muda huo lakini pia Mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza wakuu wa
wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kutoa taarifa ya
upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kila baada ya miezi mitatu lengo
likiwa ni kuhakikisha kuwa vyoo bora vinakuwepo kutumika ipasavyo muda
wote.
Malima aliwataka wakazi wa mkoa wa Mara kuachana na mila potofu ambazo
ni miongoni mwa sababu zinazochangia matumizi hafifu ya vyoo huku
akifafanua kuwa zipo baadhi ya jamii ambazo baba anashindwa kutumia choo
kimoja na watoto pamoja na wanafamilia wengine hivyo kusababisha kaya
kukosa choo
Awali Afisa afya wa mkoa wa Mara, Dk. Bumija Mhando alisema kuwa hadi
Desemba 2018 ni asilimia 55 tu ya kaya za mkoani Mara ndiyo zenye vyoo
bora huku asilimia 38 zikiwa na vyoo vya asili na asilimia saba zikiwa
hazina vyoo kabisa.
Dk. Mhando Aliongeza kuwa takwimu pia zinaonyesha ni asilimia 6 tu ya
wakazi wa Mara ndio wananawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya
kutoka chooni jambo ambalo linahitaji jitahada zaidi kuhamasisha na
kuelimsiha jamii juu ya umuhimu wa kunawa mikono mara baada ya kutoka
chooni.
Naye Mkuu wa wilaya ya Musoma, Dk. Vicent Naano alisema kuwa anakusudia
kuwachukukia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kutoza faini kuanzia
sh 20,000 kwa mkazi yeyote wa wilaya yake ambaye atashindwa kujenga na
kutumia choo ipasavyo.
Alisema kuwa kufuatia kampeni iliyoendeshwa na serikali wilayani Musoma
wakazi wengi wa wilaya hiyo waliweza kujenga vyoo huku changamoto kubwa
ikiwa ni matumizi sahihi ya vyoo hivyo kwavile wapo baadhi yao
wanajisaidia porini na ziwani.
"Sasa hivi tutaanza msako wa nyumba kwa nyumba kuangalia kama vyoo hivyo
vinatumika kwavile tumegundua kuna vyoo vimejengwa kwaajili ya ukaguzi
huku mkisema ni choo cha DC sasa nakuja kuangalia kama kweli hicho choo
kinatumika au ni cha DC", alisema Naano.
Nyakwesi Majura ni mwananchi wa manispaa ya Musoma alisema katika mila
yao hawawezi kushea choo moja na baba mkwe wake hivyo hata kama choo
kupo basi kinakuwa hakitumiki kwa kuofia kuvunja miiko iliyopo ndani ya
mila zao.
Alisema kuwa kwa sasa wanaanza kubadili tabia kutokana na elimu wanazo
zipata na kujua madhara ya kujisaidia hovyo kuwa yanaleta magonjwa ya
mlipuko na kuwa ni uchafuzi wa mazingira.
No comments :
Post a Comment