
Na Patrick Mabula - Kahama.
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga
linawashikilia watu wawili Mrisho Zabron (37) na Mgema Patrick ( 25 )
kwa tuhuma ya kujifanya Maafisa Usalama wa taifa (TSI) na kuwatapeli
watu pesa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao
amesema Zabron ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyasubi na Patrick mkazi wa
Majengo walikamtwa juzi baada ya jeshi la polisi kuwawekea mtego na
kufanikiwa kuwakamata.
"Siku ya tukio walijifanya maafisa usalama wa taifa walikwenda kwa
mfanyabiashara Abdalah Moro wa mjini Kahama aliyekuwa amefungiwa
godauni lake na TFDA na kujitambulisha maafisa usalama wa taifa
walimwomba awapatie rushwa ya shilingi milioni tatu ili aweze
kufunguliwa godauni lake lakini akatoa taarifa kwa jeshi la
polisi",ameeleza.
Kamanda Abwao ameeleza kuwa baada ya jeshi la polisi baada ya kupewa
taarifa hiyo na mfanyabiashara Moro juu watu hao waliokuwa wanajifanya
maafisa usalama wa taifa lilikwenda kuweka mtego na kufanikiwa
kuwakamata watuhumiwa wakiwa wanajiandaa kupokea kiasi cha fedha hizo
walizokuwa wameomba.
Kamanda Abwao amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi na
utakapokamilika watafikishwa mahakamani na ametoa rai kwa watu
kuwa makini na matapeli ambao wamekuwa wakitapeli wananchi kwa kutumia
taasisi hiyo nyeti ya serikali.
No comments :
Post a Comment