Saturday, June 29, 2019

Wabunge wa Upinzani Wapinga Tundu Lissu Kuvuliwa Ubunge


Baadhi ya wabunge wa upinzani nchini Tanzania wametoa maoni kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii kufuatia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kutangaza kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa kikikaliwa na Tundu Lisu wa Chadema kiko wazi.

Spika Ndugai alitangaza uamuzi huo jana Ijumaa Juni 28,2019 kabla ya kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge la Bajeti akisema Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu mbili za kutokutoa taarifa kwake (spika) na kutojaza fomu za mali na madeni kwa viongozi wa umma.

Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Godbless Lema kwenye ukurasa wake wa Twiter ameandika kuwa “Mh Spika umemvua Mh Tundu Lissu Ubunge? Moyo wangu unavuja damu....Mungu nisaidie,”

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ameandika katika ukurasa wake wa Twiter,  “Katika maisha yangu sijawahi kushuhudia unyama wa kiwango hiki,”

“Lissu alipigwa risasi mchana kweupe wakati wa vikao vya bunge,  hakuna mtu amekamatwa mpaka sasa, hakuna mtu alienda kumuona hospital akiwemo spika mwenyewe....Leo wanamvua ubunge?” ameandika Heche.

No comments :

Post a Comment