Saturday, June 29, 2019

Hifadhi ya jamii na siku ya wajane duniani


Tokeo la picha la maadhimisho ya Siku ya Wajane yaliyofanyika jijini Dodoma.Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenzwa na wajane wakati alipotembekea banda la Mtandao wa wajane Tanzania katika maadhimisho ya Siku ya Wajane yaliyofanyika jijini Dodoma.

Na Christian Gaya gayagmc@yahoo.com
Majira 28.Juni.2019
Siku ya wajane duniani kila mwaka hufanyika mwezi Juni 23. Ambapo kwa mwaka huu maandamano ya kusheherekea siku hii ya wajane Duniani yalifanyika jijini Dodoma.
Wajane na wagane pamoja na watoto wao wana wajibu wa kujua mafao ya urithi yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii kama haki yao kama aliyekuwa...
wanamtegemea alikuwa mwanachama hai wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Wanatakiwa kujua sifa zinazotakiwa ili kupata mafao hayo ya urithi, mafao yanayotolewa, mgawanyo wa pensheni hizo za urithi, pamoja na viambatanisho vinavyotakiwa wakati wa kufungua madai yao.
Baada ya kuijua, vile vile ni wajibu wao kuhakikisha ya kuwa wanafuatilia kwa kutembelea ofisi za mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii. Wategemezi wanatakiwa kufanya hivyo bila kuchoka au kukata tamaa. Utafiti unaonesha ya kuwa idadi kubwa ya wajane au wagane na watoto wao hawatambui au hawajui haki zao za mafao ya urithi. Hivyo wengi wao  hawajui ofisi za hifadhi ya jamii zilipo na hata namna ya kufuatilia hizo haki.
Mara nyingi changamoto kubwa wanayoipigia kelele wajane wengi nchini ni hali ya uchumi kuporomoka pindi wakiondokewa na wenza wao, hivyo tatizo hilo pia huongeza idadi ya watoto yatima mitaani. Baadhi ya mila za makabila fulani hapa nchini zinazofanyika katika jamii zetu huwa zinawagandamiza na kuwanyanyasa wajane, wagane na watoto wao.
Hata kama yatima wameachwa wakiwa watu wazima, wanaweza wasifahamu kwamba wanapaswa kurithi kiasi gani cha mali ya marehemu baba yao. Tatizo kama hili linaweza kujitokeza iwapo marehemu alikuwa hajagawa urithi kwa wanawe, au hakuacha wosia wowote.
Vile vile kama mama mzazi wa watoto bado yupo hai, kunaweza kutokea mgongano kati ya watoto na mama yao, wakati wa kugawana mali iliyoachwa na marehemu. Lengo la kutunga sheria inayosimamia maswala ya urithi ni kuepusha migongano kwa kuhakikisha kuwa haki ya kila anayestahili kurithi inalindwa
Ili kukwepa changamoto hizo watanzania wanatakiwa kujiunga kwa mpango wa hiari na mpango lazima yanayoendeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini na hii haijarishi kama anafanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi au sekta iliyo rasmi na hata binafsi.
Kuwepo kwa mifuko hii ya hifadhi ya jamii kunaweza kuwa msaada mkubwa kwa wajane au wagane na watoto wao pindi mwanachama mwanamke au mwanamme wa mfuko wa hifadhi ya jamii marehemu anapofariki kuwa ndio kimbilio la watu wengi wa kundi kama mwanaume au mwanawake alikuwa mwanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii
Ambapo inaweza kuwasaidia wajane au wagane hata kuanzisha miradi mbalimbali ya kuweza kuinua  kimaisha ikiwemo ya kufanya biashara ndogondogo za ujasiriamali, kama tulivyojionea mwaka huu jijini Dodoma wajane wengi wakionesha bidhaa za aina mbalimbali wakati wa kusherekea siku ya wajane duniani.
Inataja wazi ya kuwa mafao ya urithi hulipwa kwa warithi wa mwanachama wa ZSSF aliyefariki dunia akiwa bado yupo katika ajira na akiwa bado hajalipwa mafao ya uzeeni au ya ulemavu. Mafao ya urithi ni ya mkupuo tu na hulipwa warithi kwa mujibu wa sheria za mirathi ya imani ya wahusika
Mara baada ya kukamilika taratibu za hesabu, malipo kwa warithi hupitia Kamisheni ya Wakfu na mali ya amana kwa ajili ya warithi wa Imani ya Kiislamu na malipo mengine hufanyika kupitia ofisi ya Mrajisi Mkuu wa Serikali kwa ajili ya warithi wa imani ya Kikristo na nyenginezo.
Sheria hii ya ZSSF inasema ili mwanachama aweze kupata mafao ya urithi, anahitajika kuwasilisha vielelezo kama vile cheti cha uthibitisho wa kifo au kibali cha mazishi, barua ya mwajiri yenye kuthibitisha kufariki kwa Mwajiri husika na kuwaombea mafao warithi wake.
Na vielelezo vingine ni barua binafsi ya warithi au msimamizi wa mirathi ya kuomba mafao. kadi ya uanachama ya ZSSF ya marehemu, fomu ya maombi SSF 11 ambayo hupatikanwa na kujazwa mbele ya ofisa mafao katika ofisi za ZSSF.
Hapa itambuliwe ya kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kutoa mafao ya urithi kwa yatima na wajane wanaotambuliwa kisheria na kwa utaratibu unaoeleweka ni njia mojawapo ya kupiga vita mila potofu kama za kurithi na kutakasa wajane na watoto wao, ambapo mara nyingi tumeone wajane na yatima  kunyanyaswa kijinsia.
Hivyo kwa upande wa utaratibu na sheria za hifadhi ya jamii nchini zinazohusu mafao urithi utafiti unaonesha ya kuwa zinaweza kuwa rafiki kwa wajane, wagane na watoto wao.
ZSSF ilianzishwa mwaka 1998 katika awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. Salmin Amour Juma kwa lengo la kutatua changamoto mbili kuu. Awali kuisaidia Serikali katika kurahisisha upatikanaji wa mafao kwa watumishi wake kwa wakati huo. Lakini pia kuharakisha upatikanaji wa malipo hayo kwa haraka na kwa wakati muafaka.
Mfuko wa ZSSF unatekeleza majukumu yake kutokana na sheria nambari 2 ya mwaka 2005, Sheria ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2016 kwa lengo la kuufanya Mfuko wa ZSSF kuwa endelevu na kupanua wigo kwa kuwajumuisha katika wigo wa hifadhi ya jamii walio katika sekta isiyo rasmi kwa maana waliojiajiri wenyewe ambapo kwa sasa wana fursa ya kujichangia kwa hiari.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mfuko unalipa kwa wanachama wake mafao manne katika ya mafao matano yanayotajwa kwa mujibu wa Sheria.
Mafao yanayolipwa ni mafao ya uzeeni yakijumuisha pensheni na kiinua mgongo kwa wastaafu, mafao ya urithi, mafao ya ulemavu na mafao uzazi kwa wanachama wanawake.
“Aidha fao la matibabu   kwa sasa linafanyiwa tathmini na wataalamu ambalo linategemewa kuwa litakuwa fao la tano kwa mujibu wa sheria na mara mipango hiyo itakapokamilika, mfuko wa ZSSF ukishirikiana na Serikali utatoa maelekezo rasmi juu ya fao hilo la matibabu.” Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Issa Machano anafafanua zaidi.

No comments :

Post a Comment