MNYUKANO
kati ya Job Ndugai, Spika wa Bunge na Profesa Mussa Assad, Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), bado unaendelea. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Spika Ndugai amelieleza Bunge leo tarehe 16 Mei 2019 kwamba, Bunge limepokea ripoti ya ukaguzi wa hesabu katika ofisi ya CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2018.
“Kwa
mujibu wa kifungu 46, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ukaguzi wa
Umma sheria namba 11 ya mwaka 2008, hesabu za CAG yaani za ofisi ya
taifa ya ukaguzi zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka.
“Bunge
kupitia Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ina jukumu la
kuteua mkaguzi wa kukagua hesabu za ofisi hiyo. Kwa maneno rahisi, Bunge
ndio tunatafuta mkaguzi wa nje ambaye ndiye anayekagua hesabu za CAG,”
amesema Spika Ndugai na kuongeza;
“Kwa
hiyo, ukaguzi ulishafanyika huko nyuma na Kampuni ya Mkaguzi inaitwa EKI
MANGESHO KAMPANI…, imefanya kazi hiyo ya ukaguzi na imetuletea taarifa
ya hesabu zilizokaguliwa za ofisi hiyo.”
Prof.
Assad na Spika Ndugai wameingia kwenye msuguano kuanzia mwishoni mwa
mwaka jana, baada ya Pro. Assad kusema ‘Bunge ni dhaifu’ alipokuwa nje
ya nchi. Tayari Bunge limetangaza azimio la kutofanya kazi na Prof.
Assad.
Akizungumzia
taarifa hiyo Spika Ndugai amewaambia wabunge kuwa, ameona afanye hivyo
na kwamba, pamoja na CAG kuweka mezani hesabu za taasisi zingine,
taasisi hiyo hesabu zake huwa haziweki mezani.
“Nimeona
niwajulisheni ili muweze kufahamu katika hesabu zilizowekwa mezani
wakati ule, hesabu za ofisi ya CAG mwenyewe huwa haziwekwi mezani,
utaratibu wake ni huu ninaoeleza.
“Kunakuwa
na mkaguzi kutoka nje anakagua. Nawataarifu sasa bungeni kuwa,
nimeishapokea taarifa hiyo na nimeishaipitia, kuna mambo lakini
utaratibu ni kwamba, tunapeleka kwenye kamati ya PAC (Kamati ya Kudumu
ya Hesabu za Serikali),” amesema.
Spika Ndugai amesema, kwa kwa kuzingatia sheria ya ukaguzi, ripoti hiyo hiyo anaipeleka PAC ili ipitie na kuichambua.
“Mara
itakapomaliza, itawasilisha uchambuzi huo kwangu na mambo mengine
yatakayofuatia ni yale ambayo yatakuwa ya wakati huo, katika masuala ya
ukaguzi, hakuna anayebaki na hakuna anayejikagua mwenyewe, kila watu
wanaangalia wenzao,” amesema Spika Ndugai.
No comments :
Post a Comment