*Amwagiza Katibu Mkuu Kilimo atume timu
ichunguze Bodi ya Pamba
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ana imani kuwa
ununuzi wa zao la pamba utaanza mara moja kwa bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja
katika mikoa yote inayozalisha zao hilo.
Amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo kwa sintofahamu ya
bei kwa takriban ya wiki nne tangu bei elekezi ilipotangazwa Aprili 30, 2019
mkoani Shinyanga kwamba bei hiyo ianze kutumika kuanzia Mei 2, 2019.
Alikuwa akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya pamba
kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatano, Mei 29, 2019) kwenye ukumbi wa Chuo
cha Benki Kuu, jijini Mwanza. Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa
Kilimo na Viwanda, Makatibu Wakuu wa Kilimo na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wakuu wa Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara,
Shinyanga, Simiyu na Geita.
Wengine ni wawakilishi wa Wabunge wa mikoa hiyo, Makatibu
Tawala wa mikoa, Wakuu wa Wilaya zote za mikoa hiyo, na Wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya hizo. Pia kilihudhuriwa na wanunuzi wa pamba, wakulima na
maafisa wa benki kadhaa.
Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba
Serikali bado inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuwakutanisha wadau wa mazao ya
kibiashara ili yaweze kuwa na tija kwa wakulima. Alisema kazi hiyo inafanywa wa
Wizara ya Kilimo. Mazao hayo ni pamba, chai, kahawa, korosho, tumbaku na chikichi.
Pia alisema Bodi ya Pamba iachiwe jukumu la kutoa
leseni za ununuzi wa zao hilo na kwamba Wakurugenzi wa Halmashauri waliokuwa
wakifanya kazi hiyo waache mara moja. “Kuna baadhi ya Wakurugenzi wanatoa
leseni za ununuzi, lakini wenye Mamlaka ni Bodi ya Pamba. Mnunuzi nenda Bodi
ukapate leseni yako,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuwakemea baadhi ya wakurugenzi
ambao wamekuwa wakizuia wanunuzi wapya kwenye maeneo na kuendelea kuwakumbatia
wanaowataka wao. “Wakurugenzi baadhi yenu mnazuia wanunuzi wapya, mnamtaka fulani
tu. Kwa kufanya hivyo, unapungua kiwango cha kilo ambacho wakulima wako
wangeuza,” alionya.
‘Wanunuzi nendeni mkajitambulishe kwa Wakuu wa Wilaya
au Wakurugenzi ili watambue kwamba mpo kwenye maeneo yao lakini kila mnunuzi
anayo haki ya kwenda kununua pamba mahali popote hapa nchini.”
Kuhusu ubora wa pamba, Waziri Mkuu alitaka wananchi
waelimishwe ili waache kuweka maji au mchanga kwenye pamba kwa minajili ya
kuongeza uzito kwani kwa kufanya hivyo wanachafua jina la Tanzania pindi
inapopelekwa kuuzwa nje ya nchi.
Pia alitaka vyama vikuu vya ushirika vijiridhishe
kuhusu ubora wa maghala ya kuhifadhia pamba kwenye vyama vya msingi (AMCOS) kwani
kwa kufanya hivyo, itawasaidia wakulima wauze mapema pamba yao mara baada ya
kuivuna.
Kuhusu mizani, Waziri Mkuu aliiagiza wakala wa
vipimo nchini (WMA) waende wakakague mizani ya kwenye AMCOS na kwenye vinu vya kuchambulia
pamba (ginneries) kwa sbabu ya tofauti kubwa ya uzito inayojitokeza na
kuwalazimisha wakulima kulipia upotevu wa kilo hizo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe atume wakaguzi kwenye Bodi ya Pamba ili wabainishe
matumizi ya sh.100 kwa kila kilo ambazo zimekuwa zikilipwa kwenye bodi hiyo.
“Katibu Mkuu Kilimo lete wakaguzi ndani ya bodi ya
pamba, waangalie kwa kipindi cha miaka mitatu toka tulipoanza kukusanya sh. 100
kwa kilo, zimekusanywa shilingi ngapi, na zimetumika kulipia nini.
“Na Mrajisi wa Ushirika nchini ufanye ukaguzi kwenye
vyama vikuu vya Ushirika na AMCOS. Uangalie ziko ngapi na zinafanya nini. Kuna AMCOS
zina hela, je fedha hiyo imetumika kufanya nini ili kuendeleza zao la pamba. Je
zimenunua matrekta au zimelipia posho za vikao,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi Binafsi wa Pamba
(TCA), Bw. Christopher Gachuma ameshukuru Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa
kuhusu utoaji wa leseni kwani yalikuwa ni kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanunuzi
wa zao hilo.
“Suala la utoaji leseni linapaswa lianze mapema lakini kuna wengine hadi
sasa bado hawajapata leseni zao.” Aliwataka wanunuzi wa pamba waanze kununua
pamba ili msimu wa mauzo uanze kwa kasi.
No comments :
Post a Comment