Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kigwangala, wakati
akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA, kuwasalimia na
kuwaaga Watalii kutoka nchini Israel Aprili 27, 2019.
Wasanii wa kabila la Kimasai,
wakitoa burudani kwa Watalii kutoka nchini Israel Aprili 27, 2019,
kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Kigwangala, kwenye
uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA, alipofika kuwasalimia na kuwaaga
Watalii kutoka nchini Israel Aprili 27, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na Watalii kutoka nchini Israel, kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa KIA, wakati akiwaaga Aprili 27, 2019
Watalii kutoka nchini Israel,
wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa KIA, kabla ya kuondoka nchini, Aprili 27, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akimvalisha kikoi Mkurugenzi wa Kampuni ya Another World Shlomo Carmel,
iliyoleta Watalii 1000 kutoka nchini Israel, kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa KIA Aprili 27, 2019. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii
Khamis Kigwangala.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiagana na watalii kutoka nchini Israel, kwenye uwanja wa ndege wa
kimataifa wa KIA Aprili 27, 2019. Kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya
Another World Shlomo Carmel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
…………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka watalii kutoka Israel wakawe mabalozi wazuri
wa kuitangaza
Tanzania pindi wakirudi huko kwao.
Ametoa wito huo leo mchana
(Jumamosi, Aprili 27, 2019) kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA)
wakati akiwaaga watalii 274 walioondoka nchini leo mchana kurejea kwao.
Watalii hao ni miongoni mwa
watalii 1,000 waliowasili nchini tangu Aprili 20, mwaka huu na
kutembelea maeneo kadhaa ya vivutio kwenye ukanda wa Kaskazini.
Kundi la kwanza liliondoka jana
usiku, la pili leo mchana, la tatu litaondoka leo saa 10 jioni na la
mwisho litaondoka leo saa 2 usiku.
Waziri Mkuu amewaomba watalii hao
wapange muda wao na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea
mbuga nyingine za ukanda wa Kusini pamoja fukwe nzuri za Zanzibar.
“Tumefarijika sana na ujio wenu na
tunaamini mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. Tunazo mbuga
nyingine za Rubondo, Katavi, Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za
Zanzibar na mlima Kilimanjaro,” amesema.
Pia amewashukuru mawakala wa
utalii nchini pamoja na Mkurugenzi wa kampuni wakala wa utalii ya
Another World kutoka Israel Bw. Carmel Shlomo kwa kuamua kuitangaza
Tanzania kama kivutio namba moja cha utalii barani Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla aliwashukuru watalii hao kwa
kuamua kuitembelea Tanzania licha ya kuwa wangeweza kwenda maeneo
mengine yaliyo jirani na Israel.
“Natambua uchovu mlionao sababu ya
urefu wa safari kutoka Israel hadi hapa, lakini nawashukuru kwa uamuzi
wenu wa kuja Tanzania katika kipindi hiki ambacho tunafanya maboresho
kwenye sekta ya utalii ili tuweze kutoa huduma bora zaidi,” alisema.
Alisema Tanzania ina vivutio vingi
vya utalii na hii inawezekana kwa sababu iliamua kutenga zaidi ya robo
ya ardhi yake kwa ajili ya mbuga na hifadhi za taifa za wanyama.
Pia alizishukuru kampuni za utalii
za Tanzania na Israeli kwa kushirikiana kuleta watalii wengi kiasi
hicho. Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Excellent Guides, Mauly Tours and
Safaris, Matembezi, Leopard Tours and Safaris, African Queen Adventures
na TAWISA zote za kutoka Tanzania. Kamuni za kutoka Israeli ni Another
World, My Trip, Camel na Safari Company.
Kwa upande wao, baadhi ya watalii
kutoka Israel wamesema wamevutiwa na waliyaona hapa nchini na wameahidi
kurudi tena ili watembelee vivutio vingine zaidi.
Bibi Naomi Peer Moscovich na
mabinti zake Dana na Lihi wamesema wamevutiwa na wingi wa wanyama
waliowaona lakini pia wameguswa na ukarimu wa watu waliokutana nao.
“Tunaondoka na neno moja kubwa
nalo ni kwamba hatutaisahau Tanzania (we say Unforgettable Tanzania) na
tutarudi tena hivi karibuni,” alisema Dana Peer Moscovich ambaye ni dada
yake Lihi.
Hafla ya kuwaaga watalii hao
ilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii nchini, Jaji Thomas
Mihayo, Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adolf Mkenda na Wakuu
wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Mama Anna Mghwira na Bw. Mrisho
Gambo.
No comments :
Post a Comment