*Asisitiza wanaume wapime VVU ili wajue hadhi zao, wasitegemee wake zao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
wakazi wa Dodoma wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili iweze kutumika
kuokoa maisha ya wengine.
Ametoa kauli hiyo hilo leo (Jumanne,
Aprili 30, 2019) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma
waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote (UCSAF) yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere, jijini
Dodoma.
Amesema Serikali inaendelea na kampeni
ya kuhakikisha vituo vya afya na hospitali vinakuwa na
akiba ya kutosha
ya damu kwa ajili ya wagonjwa wenye kuhitaji damu.
“Tunawasihi Watanzania waende
kuchangia damu ili benki ya damu iwe na akiba ya kutosha endapo mtu
ataenda pale kufanyiwa upasuaji na akapoteza damu nyingi, au awe amepata
ajali au ameenda kujifungua, apate damu kwa haraka kutoka kwenye benki
yetu,” amesisitiza.
Akitumia wingi wa watu kwenye hafla
hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Leo hii hapa Dodoma kuna hospitali kubwa ya
Benjamin Mkapa kule UDOM, tuna vituo vya afya kama kile cha Makole vyote
vinahitaji kutoa huduma hii lakini haitoshi. Tuliagiza kila penye
mkusanyiko wa watu wengi, lazima kujengwe banda la kupima afya na
kuchangia damu.”
Akizungumziai kuhusu upimaji wa virusi
vya UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu amesema kampeni inafanyika lakini kasoro
iliyopo ni kwamba wanaojitokeza kwa wingi kupima afya zao ni wanawake na
wanaume hawapimi. “Takwimu zilizopo zinaonyesha hivyo,” amesema.
“Mimi ndiye balozi wenu akinababa
kwenye kampebi ya kitaita ya upimaji VVU. Nataka niwahimize twende leo
tukapime, tusitegemee matokeo ya vipimo vya mke. Wengi mnasubiri matokeo
ya mke, akisharudi kutoka kupima na kusema niko safi, basi na wewe
unaanza kufurahi unasema niko safi, hapana!”
“Wanaume msijidanganye, nenda ukapime
wewe mwenyewe ujijue afya yako na mkeo naye apime ajijue ili nyumba
nzima iwe na uhakika kwamba mko salama. Kwa hiyo wanaume tukitoka hapa,
twende tukapime,” alisema.
Mapema, Mkuu wa Kitengo cha Damu
Salama Mkoa wa Dodoma, Dk. Leah Kitundya alimweleza Waziri Mkuu kwamba
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ina upungufu wa damu kwa sababu kuna matukio
mengi yanayosababisha upungufu wa damu,
“Tukisema kuwa tunakusanya chupa za
kutosha, tunahitaji tuwe na chupa 1,000 hadi 1,500 za damu lakini katika
hali ya kawaida huwa tunakusanya chupa za damu 850 hadi 950 tu,”
alisema.
No comments :
Post a Comment