SUA, Morogoro
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo
Profesa. Elisante Ole Gabriel amefurahishwa na shughuli zinazofanywa na
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo hususan uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya
Wanyama.
Hospitali hiyo ni taasisi pekee
nchini inayosaidia kutoa ushauri, tiba na chanjo kwa wanyama wa kufugwa
na waporini ambao wamepewa rufaa kutoka katika Hospitali ndogo ndogo za
wanyama, taasisi za serikali na binafsi ambazo huhifadhi na kuwatunza
wanyama hao ambao hupatikana kisheria.
Akizungumza wakati wa ziara yake
ya siku moja chuoni hapo leo Aprili 23, 2019, Prof. Gabriel amesema
alipata fursa ya kuzunguka nchi za Afrika Mashariki lakini hakuwahi
kusikia uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Wanyama na hivyo kuwataka
waandishi wa habari kwa kushirkiana na kitengo cha Mawasiliano na Masoko
kuhakikisha Umma unafahamu kuhusu Hospitali hiyo kuwepo katika Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo.
“Nimefurahishwa na Hospitali ya
Rufaa ya Wanyama hapa SUA ambayo ni kwa Tanzania nzima, ni vyema
tukauhabarisha Umma kuhusu hili na ikibidi Waziri aweze kutembelea
Hoapitali hii, kiukweli nimefurahishwa sana na mambo niliyoyaona hapa
SUA na nashukuru ziara yangu hii sikukosea kuifanya hapa”. Alisema Prof.
Gabriel.
Pia aliongeza kuwa SUA inaweza
kuwa zaidi ya eneo la mafunzo kwani kuna utalii ndani yake ambapo
aliwashauri watumishi wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya
kuanzisha programu ya Utalii ambapo watu wakija kufanya mafunzo ya tiba
ya wanyama wapate kujionea mambo ya Utalii yaliyopo katika Ndaki hiyo na
hata Ndaki nyingine.
Aidha, Prof. Gabriel alipata fursa
ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo na kujionea shughuli
zinazofanywa ambapo alipata fursa ya kuona wanyama wakipatiwa tiba
ikiwemo upasuaji wakiwa katika uangalizi wa madaktari maalum wa wanyama.
“Sikuwa najua kama paka anaweza
akafanyiwa upasuaji na kukatwa mguu na bado akaendelea kuwa hai hivyo
natoa wito kwa wananchi wote kutumia Hospitali hii kuleta wanyama wao
ili waweze kupatiwa matibabu mbalimbali, mimi nimefanikiwa kuona paka
aliyefanyiwa operesheni na kukatwa mguu pamoja na mbwa ambao wote wako
katika hali nzuri”, alisema Prof. Gabriel.
Katibu Mkuu huyo pia alipata fursa
ya kuzungumza na Menejimenti ya Chuo na kuwataka kuendelea kuzalisha
wahitimu bora na kuwafanya kuwa ni wahitimu waliofundishwa kwa vitendo
zaidi kuliko nadharia huku akishauri kuwa Chuo kitoe uelewa kwa
wanafunzi kuwa sekta ya mifugo ni sekta inayoajiri zaidi ya asilimia 50
ya wataalam wa mifugo na kutambua kuwa ni vyema wajijengee hari ya
kutaka kujiari ili nao waweze kuja kuajili wengine pia.
“Ili tumuenzi Rais wetu John
Pombe Joseph Magufuli ambaye ameonyesha msukumo wa pekee ni vyema
tuhakikishe wahitimu wetu wanakuwa na uelewa kwa vitendo na si nadharia
tu ili kutatua changamoto za wanafunzi”, alishauri Prof. Gabriel.
Aliongeza kuwa chuo kinatakiwa
kuongeza nguvu katika kutoa mafunzo ya biashara (Business knowledge)
hususan katika upande wa tiba ya wanyama na Sayansi ya wanyama ili
kuwapa wataalam ujuzi wa masuala ya biashara.
“Nina hakika tukiongeza mafunzo
ya biashara kwa wataalam wetu itasaidia kupata wanafunzi wa tofauti
sana ambao mara baada ya kumaliza Chuo wakienda mtaani hawatapwaya
katika utendaji kutokana na taaluma waliyopewa kwani biashara ndio kila
kitu”, aliongeza Prof. Gabriel.
Prof. Gabriel amesisitiza Chuo
hicho kihakikishe kinawagusa wafugaji wa chini kwa kushirikiana na
Wizara kuwapeleka wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika
sehemu halisia za kujifunzia.
“Chuo kishirikiane na Wizara
pamoja na Tamisemi kuandika barua ili kuomba Wilaya mbalimbali zikubali
kuwapokea wanafunzi wetu na kuwapatia maradhi badala ya kuwaacha
wanafunzi hao kwenda mahali ambapo hawatapata nafasi ya kujifunza kwa
vitendo wakijaribu kukwepa gharama za kujihudumia wawapo katika mafunzo
na hivyo kuangalia wapi wana jamaa ambao wanaweza kupata hifadhi”,
alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Prof.
Raphael Chubunda alimshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na mchango wa
mawazo ambapo alisema kwa kiasi Chuo kimeshaanza kushughulikia baadhi ya
masuala hususani kuwa na mahali halisia pa kujifunzia na hivyo
kuanzisha mashamba darasa ya mazao ya kimkakati kwa ajili ya wanafunzi
na jamii kwa ujumla.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Mgufuli kwa kuwekea
mkazo uwezeshaji kwenye vyuo na hasa chuo chetu kwa miaka miwili
iliyopita kuna mambo makubwa ambayo huko serikali ilikuwa kama imevisusa
vyuo vyake na kubaki kama yatima na kusababisha kuchakaa kwa baadhi ya
miundombinu ya kufundishia mfano chuo chetu tunategemea mashamba na
karakana ambazo kwa sehemu kubwa zilichakaa. Kwa sasa serikali na
menejimenti ya chuo imefanya juhudi ya kupata mashamba makubwa ya chuo
yaani “Modal farms na tumepanda mazao yote ya kimkakati kama vile
zabibu, korosho pamoja na chai” alisema Prof.Chibunda.
Aidha, katika kuimarisha utoaji wa
elimu bora Chuo kimeboresha maeneo ya mifugo kama vile ngombe, samaki
na maabara kwa lengo la wanafunzi kujifunzia kwa vitendo.
No comments :
Post a Comment