Friday, April 26, 2019

MKOA WA DAR ES SALAAM KINARA KWA MAPATO


JAFOOOOOOOOOOOO JAFO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake leo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu (Julai-Machi,2019) kwa mwaka wa fedha 2018/19.
WAANDISHI
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (hayupo pichani) alipokuwa akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu (Julai-Machi,2019) kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Picha na Alex Sonna-Fullshangwe blog
………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo,amesema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa wingi wa
mapato yaliyokusanywa kwenye mikoa yote kuanzia kipindi cha Julai hadi Machi katika mwaka huu wa fedha kuwa mkoa huo umekusanya sh.bilioni 118.4.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo  alipokuwa  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu (Julai-Machi,2019) kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Hata hivyo amesema kuwa mikoa ya Katavi, Rukwa, Kigoma, Manyara na Lindi imeburuza mkia kwenye ukusanyaji mapato ikilinganishwa na jumla ya makisio kwenye halmashauri za mikoa hiyo.
Aidha amesema kuwa  Mkoa wa Dodoma umeshika nafasi ya pili kwa kukusanya wingi wa mapato yaliyofikia sh. bilioni 57.3, ukifuatiwa na Mwanza (sh. bilioni 22.9), Arusha (sh. bilioni 22.8) na Mbeya ukikusanya sh. bilioni 19.8.
“Mikoa mitano ya mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato yaliyokusanywa ni Manyara (sh. bilioni 6.5), Lindi (sh. bilioni 6.1), Rukwa (sh. bilioni 5.8), Kigoma (sh. bilioni 4.5) na Mkoa wa Katavi (sh. bilioni 3.8),” amesisitiza Jafo.
Waziri Jafo amesema kuwa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam nayo imeongoza kwa kigezo cha asilimia ambapo imekusanya asilimia 87 ya makisio, wakati Jiji la Dodoma likiongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 50.
Aidha amesema halmashauri ya jiji la Tanga imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 57 ya makisio yake, lakini pia imekuwa ya mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 8.7,”
Amezitaja Halmashauri tano za mwisho kwa kigezo cha wingi wa mapato ni Halmashauri ya Wilaya ya Madaba iliyokusanya sh. milioni 293.7 na Halmashauri ya Wilaya ya Newala (sh. milioni 268.3).
Jafo amesema kuwa nyingine  ni halmashauri ya Wilaya ya Kakonko (sh. milioni 238.6), Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe (sh. milioni 177.3) na Halmashauri ya Wilaya ya Momba imekusanya sh. milioni 170.4.
Amesema kuwa  Halmashauri ya Mji wa Kondoa imeongoza kwenye kundi la Halmashauri za Miji kwa kigezo cha asilimia ambapo imekusanya asilimia 92 ya makisio yake.
Waziri ameongeza  kuwa katika kundi hilo Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho kwa kukusanya  asilimia 12 ya makisio.
 Halmashauri ya Mji wa Geita imeongoza kwa kigezo cha wingi wa mapato kwa kukusanya sh. bilioni 5.9 na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ikiburuza mkia kwa kukusanya sh. milioni 293.9.
Jafo amesisitiza kuwa uchambuzi huo umefanyika kwa kulinganisha makisio ya mwaka wa fedha 2018/19 kwa kushindanisha halmashauri hizo, makundi ya halmashauri na kimkoa.
Hata hivyo amesema kuwa  wakurugenzi ambao halmashauri zao zimeshika nafasi ya mwisho ni vyema wakajitathimini kabla serikali haijaanza kuchukua hatua.

No comments :

Post a Comment