Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Wilaya
ya Mvomero Bw. Florian Kyombo (mwenye kaunda suti – kulia), akikabidhi
msaada wa vitabu kwa shule ya msingi Mnyanza. Kulia kwake ni Prof.
Lughano Kusiluka Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe (mwenye sare ya
kitenge) na kushoto ni Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Myanza Bw. Robert
Ngelima na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo.
Mwanafunzi wa Kidato cha sita Mark
Malekela wa shule ya Sekondari Mzumbe, akionyesha moja ya kitabu
alichotunga kwenye maadhimisho ya siku ya Vitabu Duniani yaliyofanyika
Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro. Maadhimisho hayo yalilenga
kuhamasisha usomaji na utunzi wa vitabu Duniani.
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Wilaya
ya Mvomero Bw. Florian Kyombo (mwenye kaunda suti – kushoto), kwa
pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Pro. Lughano Kusiluka
wakikabidhi msaada wa Vitabu kwa shule ya Sekondari ya Mzumbe na Adrian
Mkoba zote za Kata ya Mzumbe wakati wa maadhimisho ya siku ya Vitabu
Duniani yaliyofanyika Kampasi Kuu Morogoro.
Wakiwa katika picha ya pamoja ni
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero Bw. Florian Kyombo (mwenye
kaunda suti – katikati), Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Pro. Lughano
Kusiluka (mwenye sare ya kitenge – kulia), Mhe. Rachel Kingu Diwani wa
Kata ya Mzumbe (Kushoto), Dkt. Albogast Musabila Mkurugenzi wa Makitaba
na huduma za Kiufundi Chuo Kikuu Mzumbe ( mwenye sare ya Kitenge wa
kwanza kulia) na Dkt. Hawa Petro Tundui ( wa kwanza kushoto)
akimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma. Kwa nyuma ni baadhi
ya wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu.
………………………….
Maadhimisho ya siku ya Vitabu
Duniani yaliadhimishwa kwa aina yake na Chuo kikuu Mzumbe Aprili 23;
2019 ambapo mbali na maonyesho ya machapisho yaliyoandikwa na
Wanazuoni;
Chuo hicho kilikabidhi msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwa shule za
Msingi na Sekondari zilizopo kwenye Kata hiyo.
Mgeni rasmi katika maadhimisho
hayo alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvombero Bw. Florian
Kyombo ambaye pamoja na mambo mengine alipongeza jitihada zinazofanywa
na Chuo Kikuu Mzumbe katika kuchangia na kuboresha sekta ya elimu nchini
hususani matumizi ya teknolojia hasa kipindi hiki cha Awamu ya Tano ya
Uongozi ambapo elimu ni agenda inayopewa kipaumbele na hivyo kutolewa
bila malipo kwa ngazi ya elimu ya Awali, Msingi na Sekondari.
“Ninatoa shukrani zangu za dhati
kwa msaada wa vitabu, shelfu na elimu mnayoendelea kuitoa kwa shule
zetu kuhusu matumizi sahihi ya vitabu hivyo, sambamba na matumizi ya
teknolojia ya utunzaji. Kwangu hili ni deni kuhakikisha tunatenga bajeti
kuwezesha shule zingine za Msingi na Sekondari kwenye Kata 30 zilizopo
kwenye Wilaya ya Mvomero zinaiga mfumo huu kwa kuifanya Kata ya Mzumbe
kuwa ni ya kujifunzia.” alisisitiza.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka amesema Chuo hicho kina wajibu
wa kuhakikisha jamii inayokizunguka inanufaika na uwepo wake kwa
kusaidia katika masuala ya maendeleo ikiwemo kuinua kiwango cha elimu
kwa kujenga hamasa ya usomaji wa vitabu, kuwakuwa hiyo ndiyo mbinu pekee
inayoweza kuwapatia Wanafunzi maarifa ya kutosha na kuweza kufikia
ngazi zote za elimu hadi Chuo Kikuu.
Amesema “ Mpango wa kuzifikia na
kutatua changamoto za Shule za Msingi na Sekondari kwa jamii
inayotuzunguka ni endelevu na ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati
wa nne (IV) wa Chuo Kikuu Mzumbe ambapo kwa awamu hii, tumetoa Vitabu
vya kiada na ziada kwa shule za Msingi Tangeni, Mnyanza,Vikenge,
Masanze, Changarawe na Mzumbe na shule tatu za Sekondari ambazo ni
Mongola,Askofu Adrian Mkoba na Mzumbe; na tayari tumetoa msada wa
Komputa na kutoa mafunzo ya matumizi ya programu mbalimbali ili
kuziwezesha shule zetu kuendeshwa kisasa kwa kutoa mafunzo yanayoendana
na wakati tulionao”.
Aidha; ameahidi Chuo Kikuu Mzumbe
kuendelea kuwa chachu katika kuhamasisha usomaji na utunzaji vitabu
wenye lengo la kurithishana elimu na ujuzi kwa manufaa mapana ya Taifa.
Siku ya Vitabu Duniani
huadhimishwa kila mwaka Aprili 23; kwa lengo la kuhamasisha usomaji wa
vitabu na kuwaenzi watunzi wa Vitabu duniani kote.
No comments :
Post a Comment