Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana akimkabidhi zawadi
Sajenti mstaafu wa Polisi Rukia Msofe wakati wa sherehe ya kuwaaga
wastaafu iliyoandaliwa na TPF NET Arusha na kufanyika bwalo la Maofisa
wa Polisi lililopo jijini hapa (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi
Arusha)
Baadhi ya Polisi wanawake ambao
ni wanachama wa TPF NET Arusha wakifungua Champaign wakati wa sherehe ya
kuwaaga wastaafu waliotumikia Jeshi hilo iliyofanyika katika ukumbi wa
Bwalo la Maofisa wa Polisi. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
Bi. Mary Simbano ambaye alikuwa
Mhasibu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Arusha, akipewa zawadi binafsi na
wanachama wa TPF NET Arusha wakati wa sherehe za kuwaaga wastaafu ambao
ni askari na watumishi raia waliokuwa wanafanya kazi mkoani hapa.
(Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
Baadhi ya wageni waalikwa
wakihudumiwa chakula wakati wa sherehe ya kuwaaga wastaafu ambao ni
askari na watumishi raia iliyoandaliwa na TPF NET Arusha (Picha na
Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha).
………………………………………………………………………………….
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Askari
pamoja na watumishi raia waliolitumikia Jeshi la Polisi mpaka kufikia
kustaafu wametakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kutoa
taarifa mbalimbali zitakazosaidia kupambana na uhalifu.
Wito
huo umetolewa na Kamanda mpya wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana jana usiku, katika
sherehe ya kuwaaga wastaafu hao
ambao ni Mkaguzi mmoja, askari wa vyeo
mbalimbali 10 pamoja na watumishi raia wawili iliyofanyika katika ukumbi
wa Bwalo la Maofisa wa Polisi uliopo jijini hapa.
“Ninyi
ndugu zetu tunaomba muendelee kutusaidia katika azma yetu ya kupambana
dhidi ya uhalifu na wakati wowote mlango ya ofisi yangu upo wazi kwa
ajili ya kuwasikiliza”. Alisema Kamanda Shana ambaye aliwasili mkoani
hapa juzi usiku akitokea Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Aidha
kamanda Shana aliahidi kuwaunga mkono TPF NET mkoani hapa na kuwataka
wanawake wasikubali kunyanyaswa na kujiona wanyonge bali wanatakiwa
kusonga mbele kwa ajili ya maendeleo ya familia zao huku akitoa mifano
ya baadhi ya nafasi za juu za wanawake ambao wapo katika idara na
taasisi mbalimbali na wameonekana wakifanya vizuri zaidi kiutendaji.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF NET) mkoa wa
Arusha Mrakibu wa Polisi Namsemba Mwakatobe alisema kwamba, wameamua
kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuunganisha sherehe ya kuwaaga
wanawake wenzao pamoja na kuwapa zawadi mbalimbali.
Alisema
baadhi ya wastaafu hao katika kipindi chao cha utumishi walikuwa walimu
wa askari na watumishi raia waliopo hivi sasa hali ambayo imesaidia
kuendelea kupata kizazi kingine kinachofanya kazi kwa ufanisi na uweledi
wa hali ya juu.
Akizungumza kwa niaba ya
wenzake, mmoja wa wastaafu Bi. Azama Libundilo ambaye alikuwa na cheo
cha Staff Sajenti alisema kwamba kitendo kilichofanywa na wanamtandao
huo pamoja na viongozi wa Polisi mkoa,cha kuwathamini wastaafu kinapaswa
kuigwa na ofisi zote ambazo hazina utamaduni huo kwani kinawatia moyo
nakujiona kwamba bado ni familia ya jeshi hilo.
No comments :
Post a Comment