Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza jitihada za Serikali katika
kupambana na utapiamlo ikiwa ni pamoja na kila mkoa kuandaa bajeti ya
lishe wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Binti Mfalme wa
Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe duniani, Sarah Zeid (hayupo
pichani), Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Khatibu Kazungu na
kulia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti wa Wizara hiyo Dkt. Charles
Mwamwaja.
Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni
balozi wa masuala ya lishe duniani, Sarah Zeid, akieleza
anavyofurahishwa na Serikali ya Tanzania inavyosimamia suala la lishe,
wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), kushoto ni Mwakilishi wa
Shirika la Chakula Duniani- WFP nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula
la Umoja wa Mataifa (WFP) Bw. Michael Dunford, akieleza utayari wa
Shirika hilo kuisaidia Tanzania katika masuala ya lishe, wakati wa
Mkutano kati ya Binti Mfalme wa Jordan, Sarah Zeid (kushoto) na Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani),
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili
kulia), na Ujumbe wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP),
ukiongozwa na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya
lishe duniani, Sarah Zeid (wa pili kulia) katika mkutano kuhusu lishe,
uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akipeana mkono na Binti Mfalme wa Jordan
ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto),
baada ya kumalizika mkutano kuhusu Lishe uliofanyika katika ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Binti Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi
wa masuala ya lishe Duniani, Sarah Zeid (kushoto), wakifurahia jambo
katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Shirika la Chakula
Duniani- WFP, baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya pande hizo
mbili katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
(Picha na Peter Haule, Wizara ya Fedha na Mipango)
…………………………..
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na
Binti wa Mfalme wa
Jordan, Sarah Zeid, ambaye ni Mwanaharakati wa masuala ya lishe,
wanawake na watoto Duniani, jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao, Dkt.
Mpango, alimweleza Princess Sarah Zeid kwamba Tanzania bado inakabiliwa
na changamoto ya masuala ya lishe, utapiamlo na udumavu wa watoto licha
ya nchi kuwa na chakula cha kutosha.
Dkt. Mpango alisema kuwa iwapo
eneo la lishe halitasimamiwa kikamilifu Taifa litazalisha watoto wenye
udumavu wa ubongo na kusababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na
utendaji hafifu wakiwa katika shughuli mbalimbali.
Alisema ipo mikoa ambayo
inazalisha mazao mengi kama Mbeya na Njombe lakini ina kiwango kikubwa
cha watoto wenye utapiamlo, na kutoa wito kwa kila mtanzania kuhakikisha
anaangalia ni chakula gani kinahitajika kwa ajili ya lishe ya watoto na
wakinamama wajawazito ili kupunguza udumavu na vifo vya mama wajawazito
na watoto wachanga.
Aidha amempongeza Mwana wa Mfalme
wa Jordan, Sarah Zeid, kwa kampeni yake anayoifanya duniani kote
kupambana na vifo vya wakinamama wajawazito na watoto kwa kuwa mchango
wa wanawake ni mkubwa katika jamii ikiwemo uzalishaji mali.
Alisema idadi ya wanawake nchini
Tanzania ni asilimia 51 ya idadi ya watu wote wanaokadiriwa kufikia
milioni 55 ambapo mchango wako katika sekta mbalimbali za uchumi umekuwa
mkubwa hivyo jitihada za kuwalinda zinahitajika.
Alimweleza Binti Mfalme wa Jordan,
Sarah Zeid kwamba kwa kutambua umuhimu wa lishe serikali imelivalia
njuga suala la lishe kwa kutenga bajeti kila mwaka katika kila wizara na
kwamba fedha hizo zimewekewa wigo zisitumike kwa matumizi mengine.
“Nimeziagiza Wizara, Mikoa na
Halmashauri zote nchini kutumia fungu lililotengwa kwa ajili ya lishe
kwa matumizi yaliyopangwa ili kuhakikisha watanzania wanaimarika kiafya
na kushiriki kikamilifu katika Shughuli za Maendeleo” Alisema Dkt.
Mpango.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa
Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Mkutano kati yake
na Mwana wa Mfalme wa Jordan ambaye ni balozi wa masuala ya Lishe Dunia,
Sarah Zeid na
Kwa upande wake Mwana wa Mfalme wa
Jordan, Sarah Zeid, ambaye aliambatana na Mwakilishi wa Shirika la
Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) nchini Tanzania, Bw. Michael Dunford,
ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake katika kupambana na
utapiamlo unaosababishwa na ukosefu wa lishe.
Amewataka watanzania kuhakikisha
suala la Lishe linapewa kipaumbele na kila mmoja kwa manufaa ya Taifa
na Dunia kwa ujumla na kwamba atahamasisha jumuiya ya kimataifa
kuchangia jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la lishe, na vifo
vya wanawake wajawazito na watoto.
Naye Mwakilishi wa Shirika la
Chakula la Umoja wa Mataifa-WFP nchini Tanzania Bw. Michael Dunford,
amesema kuwa shirika lake linatambua mchango mkubwa wa Serikali katika
kupambana na masuala ya lishe duni na shirika lake litaendelea
kushirikiana na nayo ili kufikia malengo yanayotarajiwa.
No comments :
Post a Comment