Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akizungumza
jambo na wafanyakazi wa maabara alipotembelea maabara hiyo kwa ajili ya
kuangalia mashine mpya za uchunguzi wa vipimo vya magonjwa ya moyo
zilizofungwa. Watatu kulia kutoka kwa Prof. Mahalu ni mjumbe wa bodi
Dkt. Donan Mbando.
Watoto wanaotibiwa katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa wanacheza gemu kama walivyokutwa
na mpiga picha wetu. Watoto wawili kati yao wamefanyiwa upasuaji wa
bila kufungua kifua na wawili wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu na mjumbe
wa bodi hiyo Dkt. Donan Mbando wakitoka kuangalia wodi mpya ya watoto
wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu na mjumbe wa
bodi hiyo Dkt. Donan Mbando wakiangalia chumba cha wagonjwa walioko
katika uangalizi maalum (ICU) kilichopo katika wodi mpya ya watoto
wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati. Chumba
hicho kikianza kufanya kazi kitakuwa na vitanda nane na kuweza
kurahisisha kutoa huduma kwa watoto wanaohitaji matibabu ya dharula.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu akiangalia
(medical gas bed head panel) mahali pa kuchomeka mashine ya kutolewa
hewa ya matibabu kwenda kwa mgonjwa katika wodi mpya ya kulipia ya
watoto wenye magonjwa ya moyo ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati.
Picha na JKCI
………………………..
Na Mwandishi Maalum
Kuongezeka wa idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa vipimo na uzibuaji wa mishipa ya damu ya
moyo ambayo imeziba kupitia mtambo wa Cathlab ni ishara kuwa watu wengi wanahitaji kupata huduma hiyo.
Hayo
yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akisoma ripoti ya utendaji kazi wa
Taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba kwa
bodi ya Wadhamini.
Prof. Janabi alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2016 hadi 2018 katika mtambo wa Cathlab wameona zaidi ya wagonjwa 2389 ambao waliwafanyiwa vipimo na kuwazibua mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba.
“Kupitia mtambo huu tunafanya upasuaji wa moyo wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja. Kwa
mwaka jana pekee tulifanya upasuaji kwa wagonjwa 1056 na kuvunja rekodi
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati”, alisema Prof. Janabi.
Alisema hivi sasa madaktari wa magonjwa ya moyo kwa watoto kupitia mtambo huo wa Cathlab wameanza kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba.
“Kipindi
cha nyuma watoto walikuwa wanafanyiwa upasuaji huu na madaktari wageni
hii ilitokana na kutokuwa na daktari wa kutoa huduma hiyo katika Taasisi
yetu. Mwaka jana daktari wetu mmoja aliyekuwa anasoma Afrika ya Kusini
amerudi baada ya kumaliza masomo yake na anafanya upasuaji siku ya
Jumatano”,.
“Tumetenga
siku moja kwa wiki ambayo ni jumatano watoto wanafanyiwa upasuaji wa
kuziba matundu na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba, uhitaji ni mkubwa
na mtambo uliopo ni mmoja. Kuna haja ya kuwa na mtambo mwingine wa
Cathlab ili wagonjwa wengi wenye uhitaji wa huduma hii waweze kuipata”,
alisema Prof. Janabi.
Katika
hatua nyingine Prof. Janabi alisema mwezi wa sita mwaka huu Madaktari
Afrika kutoka nchini Marekani watakuja nchini kupanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuchangia fedha za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Prof. William Mahalu
aliipongeza menejimenti na wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo kwa kazi
nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu alisema kufanya vizuri kwa mtambo wa Cathlab kunaonesha kuwa watu wengi wanahitaji huduma hiyo na wao kama bodi wameona kunahaja ya kuongeza mtambo wa pili wa Cathlab ili wagonjwa wengi wapate huduma hiyo.
“Mmetuambia hivi karibuni mmesaini mkataba wa makubaliano ya kuletwa
kwa wagonjwa kutoka nchi ya Malawi na Visiwa vya Zanzibar kwa ajili ya
matibabu, hongereni sana. Endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kujituma
ili watu wengi zaidi wafaidike na huduma mnayoitoa”, alisema Prof.
Mahalu.
Alisema miaka minne au mitano ijayo wataalamu kutoka nje ya nchi wanaokuja kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo watakuja nchini kujifunza kutoka kwa watanzania baada ya wao kuja kutoa msaada.
Prof. Mahalu alimalizia kwa kuwataka wataalamu wa magonjwa ya moyo kufuatilia maendeleo ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo pindi wanaporuhusiwa kurudi nyumbani.
No comments :
Post a Comment