Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha
fedha za kigeni jijini Dar es Salaam na kubaini kwamba maduka mengi yanaendesha
biashara hiyo pasipo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji wa huduma
ya kubadilisha fedha za kigeni.
Kufuatia ukaguzi huo, Benki Kuu ya Tanzania imeanza utaratibu wa
kufuta leseni za maduka yote yaliyokutwa yanaendesha biashara hiyo bila
kuzingatia masharti ya leseni. Zoezi hili linaendelea.
Mnamo mwezi Desemba mwaka 2018, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi
wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni nchini kote na kubaini kuwa mengi
hayakidhi matakwa ya kisheria ya biashara hiyo. Hivyo, iliyaandikia maduka hayo
kuyataka kutoa maelezo kwa nini yasifutiwe leseni kutokana na ukiukaji huo.
Hatua zilizochukuliwa jana zinatokana na tathmini ya taarifa ambazo Benki Kuu
ya Tanzania ilizipokea kutoka kwa waendeshaji wa maduka hayo.
Aidha, kama
ilivyoelezwa katika taarifa za Benki Kuu ya Tanzania za mwezi Novemba 2018 na
tarehe 31 Januari 2019, huduma za kubadilisha fedha za kigeni zinaendelea
kupatikana katika mabenki na taasisi za fedha nchini kote pamoja na maduka ya
fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).
Benki Kuu ya Tanzania
inapenda kuutahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa
fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali, ikiwemo kuibiwa au kupewa fedha
bandia. Aidha, utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma
zisizo halali (black-market).
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
No comments :
Post a Comment