Friday, January 11, 2019

WATUMISHI WA TASAF WAELEKEZWA KUZIHUDUMIA VIZURI KAYA MASKINI ILI KUZIWEZESHA KAYA HIZO KUJIKIMU KIMAISHA NA KUONDOKANA NA UMASKINI


IMG_0001
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipowatembelea ofisini kwao jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
IMG_0002
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akieleza  majukumu ya taasisi yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)  wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa TASAF kilichofanyika Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es Salaam chenye lengo la kuhumiza uwajibikaji.
IMG_0003
Baadhi ya watumishi wa Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipowatembelea ofisini kwao jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
IMG_0004
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) mara baada ya kuzungumza na watumishi wa mfuko huo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
…………………………
Watumishi wa Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) wametakiwa kuhakikisha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  wanahudumiwa vizuri kwa kupata ruzuku zao kwa
wakati ili kuziwezesha kaya hizo kujikimu kimaisha na kuondokana na umaskini.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa TASAF makao makuu katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la  kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya TASAF na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, kwa kuwahudumia vizuri wanufaika hao, TASAF pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  itapata baraka za Mwenyezi Mungu ambaye kupitia vitabu vyake vitakatifu ameelekeza kuwasaidia maskini na pia watakuwa mfano bora wa kuigwa na nchini nyingine barani Afrika kwa kutekeleza vema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa TASAF kuwa tayari muda wote katika kuhakikisha kaya zote maskini  zinapata stahili zao kwa wakati na kufurahia matunda na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuziwezesha kaya maskini kuondokana na umaskini.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameitaka TASAF kuhakikisha inaweka taratibu madhubuti za kisheria zitakazowaadhibu na kuwadhibiti wote  watakaobainika kufanya udanganyifu kujipatia fedha za mpango wakati hawana sifa za kuwa wanufaika, lengo likiwa ni kujenga nidhamu katika jamii ili fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ziwafikie walengwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anavyotaka.
Katika kutekeleza azma hiyo, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa TASAF kufanya kazi kwa ari na uzalendo mkubwa na kuipongeza TASAF kwa jitihada na mafanikio waliyoyapata katika kuzinusuru kaya maskini mpaka hivi sasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amemhakikishia Mhe. Dkt. Mwanjelwa kuwa, atahakikisha anasimamia vizuri utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kama alivyoelekeza,  ili uwe ni mpango bora zaidi katika bara la Afrika, na kuongeza kuwa, hadi sasa, tayari mpango umeonekana kuwa ni miongoni mwa mipango bora barani Afrika kwani umeweza kuboresha maisha ya kaya maskini ambapo utekelezaji wake umewezesha kuzitambua kaya maskini, umesimamiwa vizuri, malipo yanafanyika kwa wakati na hakuna ubadhilifu mkubwa wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya wanufaika.
Akithibitisha ubora wa mpango, Bw. Mwamanga amesema, hivi sasa Rais wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, anapozungumzia programu za kupambana na umaskini, haachi kuutaja Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa nchini Tanzania kuwa ni bora na unasimamiwa vizuri.
Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. John P. Magufuli aliyejipambanua kwa vitendo kuwajali wanyonge, imedhamiria kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kuwafikia walengwa  katika kaya zote maskini nchini ili walengwa hao waweze kunufaika na kuboresha maisha yao.

No comments :

Post a Comment