Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati)
akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka Benki ya NMB na
menejimenti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua
jambo wakati wa kikao na maafisa kutoka Benki ya NMB na menejimenti wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani) kuhusu uwekezaji katika sekta
ya maziwa
Meneja Mwandamizi kutoka Benki ya
NMB idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi anyeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel
(hayupo pichani) juu ya uwekezaji wa sekta ya maziwa na Benki ya NMB
………………………
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Benki
ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini
kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa kutokana na
taarifa
iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP)
Prof. Gabriel amebainisha hayo leo
(31.01.2019) Jijini Dodoma, akiwa kwenye kikao na maafisa kutoka idara
ya kilimo ya Benki ya NMB, waliofika ofisini kwake kumwelezea mikakati
ya Benki ya NMB ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya
maziwa lengo likiwa ni kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na
Shirika la Chakula Duniani ni kwamba kwa wastani angalau mtu anatakiwa
walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa lakini kwa bahati mbaya
kwa watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa
sana.” Alisema Prof Gabriel
Prof. Gabriel amesema Benki ya NMB
inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia
Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta
ya mifugo na uvuvi, ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo
maziwa yanatumika ipasavyo.
Katika kikao hicho ambacho
kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Katibu mkuu huyo pia amesema ni wakati muafaka kwa Benki ya NMB
kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inawaletea
maendeleo wafugaji, hususan wafugaji wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na
wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa
kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.
Aidha Prof. Gabriel amesisitiza
umuhimu wa kufanyika kwa tafiti kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa
kushirikiana na Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo ili tafiti hizo
ziweze kufanyiwa kazi na kuleta matokeo chanya kwa wafugaji.
“Ningependa sekta hii ya mifugo,
iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa tukifanya hizo tafiti
tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika katika maendeleo ya
wafugaji kwa sababu lengo siyo tu kufanya jambo, lakini liwe jambo
ambalo linaweza kugusa maisha ya wafugaji.” Alisema Prof. Gabriel
Katika kikao hicho pia Katibu Mkuu
Prof. Gabriel ameshauri uwepo wa mahusiano ya karibu kati ya Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Benki ya NMB na taasisi za elimu ya juu, ili
kuhakikisha tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na wanafunzi ziweze
kutumika katika kuleta mabadiliko na kuleta manufaa kwa wafugaji, badala
ya tafiti hizo kuwekwa katika maktaba za vyuo hivyo pekee.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi
wa Benki ya NMB kutoka idara ya kilimo Bw. Carol Nyagaro amesema
kutokana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Magufuli pamoja na utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewalazimu
benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia
sekta mbalimbali.
“Kutokana na kasi ya Mheshimiwa
Rais Dkt. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia
maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo.” Alisema
Bw. Ngayaro
Aidha Bw. Nyagaro amesema Benki ya
NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya
samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi
karibuni.
Bw. Nyagaro amemueleza pia Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante
Ole Gabriel, kuwa Muunganiko wa Vyama vya Ushirika Vikuu vya Maziwa
Duniani unatarajia kufanya mkutano wake hapa nchini Tarehe 25 na 26
Mwezi Februari mwaka 2019 kwa kushirikiana na Benki ya NMB lengo kuu
likiwa ni kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika sekta ya maziwa hapa
nchini.
Amefafanua kuwa muunganiko huo
wenye nchi wanachama 95 ambao unafanya biashara ya takriban Dola za
Marekani Bilioni 200 kwa mwaka, umeichagua Tanzania kwa ajili ya kufanya
majadiliano kwa kuhusisha wadau wa sekta ya mifugo ili kuwekeza katika
sekta ya maziwa.
Amesema mkutano huo pia utaainisha mambo ambayo tayari yalishafanyiwa tafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mipango hiyo.
No comments :
Post a Comment