Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura na wanaoishi kwenye kata Sita za Tanzania Bara, kujitokeza
kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Desemba 2 mwaka huu ili
kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani
miaka miwili ijayo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage wakati akisoma
risala ya uchaguzi mdogo wa Udiwani unaohusisha kata za Miteja, Kivinje
au
Sigino , Somanga na Mitole katika Halmashauri ya Kilwa, kata ya
Muhinda katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Kata ya Nkoanekoli
katika Halmashauri ya wilaya ya Meru.
“Wapiga Kura wapatao 31,818
wanatarajiwa kupiga Kura kuwachagua Madiwani katika Kata 6 za Tanzania
Bara na uchaguzi huo utafanyika katika Vituo 91 vya Kupigia Kura ambako
ndipo Wapiga kura walijiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa
Rais,Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015.
Aliwataka kwenda kupiga kura
bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi kwani chini ya Kanuni ya 3.1 (b)
ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015,
Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani
na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi.
Mbali na wito huo, Jaji Kaijage
aliwataka wananchi, vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi
kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na
utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.
Jaji Kaijage alivisisitiza vyama
vya siasa kufanya mikutano ya kampeni inatakiwa kufikia mwisho leo
Jumamosi saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni na baada ya muda huo,
vyama, wagombea na mashabiki waache kufanya kampeni za aina yoyote, kama
vile kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni, vipeperushi,
bendera, mavazi na vitu vingine visivyokubalika katika siku ya Uchaguzi.
“Aidha, wananchi waheshimu
Sheria za Nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na
kutangaza matokeo. Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa
Sheria na Taratibu za Uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye
mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.”,
alisema Jaji Kaijage na kuongeza kuwa:
“Vivyo hivyo, Viongozi wa Vyama
vya Siasa, Wagombea au wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na
vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu katika vituo vya Kupigia,
Kuhesabia na Kujumlishia Kura.”
Jaji Kaijage aliwataka wapiga
kura kuondoka kwenye maeneo ya kituo cha kupigia kura mara baada ya
kupiga kura na kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya
vituo vya kupigia kura kwani vyama vya siasa vimeweka mawakala vituoni
ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
Mwenyekiti huyo wa NEC,
alivikumbusha vyama vya siasa, wagombea, wananchi na watendaji wa
uchaguzi kwa ujumla kuzingatia na kuheshimu matakwa na masharti ya
Sheria za Uchaguzi, Sheria za Nchi, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi wakati
wa Upigaji Kura, Kuhesabu, Kujumlisha Kura, na Kutangaza matokeo.
Alisema upigaji kura utafanyika
kuanzia saa moja kamili asubuhi na kumalizika saa kumi kamili jioni
katika vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na
kwamba watakaokuwepo kwenye mstari kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia
saa kumi kamili jioni wataruhusiwa kupiga kura.
Hata hivyo, alibainisha kuwa
watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu waliomo kwenye Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura kwenye Kata husika na wana kadi ya mpiga kura na wale
waliopoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa
wataruhusiwa kupiga kura kutumia Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au
Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) kwa sharti kuwa majina yaliyomo kwenye vitambulisho hivyo
yafanane na yale yaliyomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Ni wajibu wa vyama vya siasa
vinavyoshiriki katika uchaguzi kuweka mawakala katika vituo vyote vya
Kupigia na Kujumlishia Kura kwa utaratibu ambao tulikubaliana na umekuwa
ukitumika katika chaguzi za hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Tume na
Vyama vya Siasa tarehe 10/07/2018 uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa
wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam, na maelekezo
kuhusiana na utaratibu huo kutumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi.”,
alikumbusha Jaji Kaijage.
Hata hivyo, alisema mawakala hao
wanaruhusiwa kuwepo katika Vituo vya Kupigia Kura na wanatakiwa kufuata
na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika
kipindi chote cha kupiga, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza
matokeo.
No comments :
Post a Comment