Saturday, December 1, 2018

MANYARA YAZIDI KUNG’ARA KWA MAENDELEO-MNYETI


1
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa akisoma taarifa ya maendeleo ya mkoa huo kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo.
2
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa huo (RCC) Mjini Babati. 
3
Meneja wa Tanroads Mkoani Manyara mhandisi Bashiri Rwesingisa akielezea taarifa ya utekelezaji wa matengenezo na ukarabati wa barabara za mkoa huo Mjini Babati. 
…………………………
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti amesema mkoa huo unazidi kung’ara na kupiga hatua kwenye sekta mbalimbali ya maendeleo, hivyo viongozi waendelee kuwatumikia zaidi wananchi. 
Mnyeti ameyasema hayo mjini Babati kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC). 
Alisema kwenye makusanyo ya ndani mkoa huo umeshika nafasi ya pili kitaifa katika kipindi hiki cha robo mwaka. 
Alisema kwenye miradi ya maendeleo iliyokaguliwa na mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu wamefanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa kwani miradi yao ilikubaliwa na ilipitishwa yote, hakukuwepo uliokataliwa. 
Alisema kwenye makusanyo ya mamlaka ya mapato nchini (TRA) mkoani humo lengo lilikuwa kukusanya shilingi bilioni 6.453 kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, wamekusanya shilingi bilioni 6.695 sawa na asilimia 103.8 ya lengo. 
“Katika mwaka huu wa fedha tumepiga hatua ya maendeleo katika ukusanyaji wa mapato ambapo Halmashauri zimekusanya shilingi 5,464,290,534.38 sawa na asilimia 38 ya lengo la mwaka,” alisema Mnyeti. 
Alisema kwenye agizo la kila mkoa kuwa na viwanda vipya 100 wamefanikiwa kwenye hilo kwani hata Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo alisema mkoa wa Manyara upo kwenye tatu bora kwa kuwa na viwanda vipya. 
“Kwenye viwanda vipya tumefanikiwa mno na katika hili najua tunapambana na mkoa wa Pwani, kwani huku kuna viwanda vinalipa kodi kubwa serikalini na vimetoa ajira nyingi kwa wananchi,” alisema Mnyeti. 
Alisema hali ya elimu ipo vizuri kwani kuna ongezeko la watoto wakuandikishwa kuanzia darasa la kwanza na kidato cha kwanza baada ya sera ya elimu bila malipo kuanza kutekelezwa. 
“Lengo la mkoa la kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali lilikuwa 46,709 ila wameandikishwa 42,989 sawa na asilimia 92 na darasa la kwanza lengo lilikuwa 52,923 na wameandikishwa 54,496 sawa na asilimia 107.4,” alisema Mnyeti. 
Alisema ongezeko hilo limekwenda sambamba na ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kutoka asilimia 59. 18 mwaka 2015 hadi asilimia 70.79 mwaka huu. 
Alisema kwa upande wa kidato cha nne ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 72 mwaka 2015 hadi asilimia 82.53 mwaka huu. 

No comments :

Post a Comment