Sunday, November 4, 2018

SBFIC KUWAPIGA MSASA WAJASIRIAMALI, TAASISI ZA FEDHA


1
MKURUGENZI Mkaazi wa Shirika la Savings Bank Foundation for International Cooperation Steven Noel Safe akizungumza kwenye hafla ya  kufunguliwa kwa ofisi za shirika hilo lisilo la kiserikali katika eneo la Bwiru , Ilemela jijini Mwanza.kushoto kwake ni Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba ya Tubingen Ujerumani Dr. Christoph Gogler ambaye alikuwa mgeni rasmi. Wa kwanza kushoto ni Meneja miradi wa SBFIC Mwanza, Tom.
2
Mtendaji Mkuu wa Banki ya Akiba ya Tubingen Ujerumani Dr. Christoph Gogler akiangalia machapisho yanayotumika kutoa elimu ya kuweka akiba kwa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi huku Mkurugenzi Mkaazi wa SBFIC Steven Noel Safe akimpa maelezo kuhusiana na machapisho hayo.Kulia wa kwanza ni Mtendaji Mkuu wa taasisi ya Self Micro Finance Fund,Mudith Cheyo.Shirika hilo linajenga miradi endelevu na kutoa elimu na kutafuta ufumbuzi bora wa masuala ya kifedha kwenye taasisi na vyama vya kuweka na kukopa.
3
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba ya Tubingen Ujerumani Dr. Christoph Gogler akikata utepe kufungua ofisi  huku Mkurugenzi Mkaazi wa SBFIC Steven Noel Safe , mwenye kinasa sauti akishuhudia (kulia wa kwanza).
 
4
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba ya Tubingen Ujerumani Dr. Christoph Gogler ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa ofisi za SBFIC jijini Mwanza akikata keki.Wa kwanza kulia anayeshuhudia ni Meneja miradi wa SBFIC Mwanza, Steven Noel Safe.
5
Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba ya Tubingen Ujerumani Dr. Christoph Gogler ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa ofisi za SBFIC jijini Mwanza akilishwa keki na Leah Michael, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Karagwe.Wa kwanza kulia anayeshuhudia ni Meneja miradi wa SBFIC Mwanza, Steven Noel Safe.
Picha zote na Baltazar Mashaka
………………………
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHIRIKA la Savings Bank Foundation for International Cooperation (SBFIC) liko kwenye mikakati ya kutoa elimu (mafunzo) ya fedha kwa taasisi ndogo ndogo za kifedha nchini ili
kutafuta ufumbuzi bora wa masuala ya kuweka na kukopa fedha.
Pia shirika hilo lisilo la kiserikali linalenga kujenga uhusiano wa muda mrefu utakaoliwezesha kushirikiana na taasisi hizo kukuza biashara na kujenga miradi yao itakayokuwa endelevu hata baada ya wafadhili kuondoka .
Mkurugenzi Mkaazi wa SBFIC nchini, Steven Noel Safe akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye hafla ya ufunguzi wa ofisi za shirika hilo lisilo la kiserikali,alisema wana mkakati wa kuwafundisha  walimu wa walimu watakaotoa elimu kwa wananchi hasa wajasiriamali namna ya kuweka na kukopa kwenye taasisi za fedha.
Alisema mkakati utakaoanza mwakani unawalenga walimu wa masuala ya elimu ya fedha hasa wa shule kwa ajili ya wanafunzi, maofisa ushirika kwa ajili ya vyama vya kuweka na kukopa na maofisa maendeleo ya jamii watakaoelimisha vikundi vya kijamii vinavyokopa kwenye halmashauri.
Safe alieleza kuwa wanataka kuwafikia wananchi wengi hivyo elimu hiyo ya kuweka na kukopa itatolewa na watalaamu waliobobea kwenye masuala ya fedha kutoka Ujerumani na nchi zingine kwa taasisi ndogo ndogo za MFIs ,Vicoba,Saccos, wakulima na wajasiriamali ili kutafuta ufumbuzi bora wa kifedha na familia kuweza kupanga bajeti ya familia.
“Changamoto kubwa ni Watanzania tunapopata miradi tusifikirie itadumu milele,tunatakiwa tuifanye kwa weledi ili tuendelee.Pia tumezoea wageni wanaotoa posho na hatutaki kuchangia chochote na wakiondoka miradi mingi inakufa na hakuna maendeleo yoyote.Kwa elimu tunayotoa tunataka mwananchi ajue kila kitu ili achague mwenyewe akakope wapi kwa riba nafuu,”alisema Safe.
Mkurugenzi huyo Mkaazi wa SBFIC alieleza kuwa kukiwa na ufanisi na ubora katika taasisi ndogo ndogo za fedha kutachangia kukuza maendeleo ya kiuchumi ya nchi, kwa kuwa uchumi mkubwa hujenga ajira na kukuza elimu ambayo ni muhimu kwa Tanzania ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati.
“Tumeanza kufundisha wanafunzi wa shule za sekondari na msingi namna ya uwekaji fedha na kuhusisha jamii nzima kwa kuwajengea uelewa wa masuala ya Financial Inclusion (fedha).Tumezisaidia taasisi washirika wetu juu ya masuala na mipango endelevu ya miradi yao, mikakati na utawala bora na mafunzo katika kuendesha miradi hiyo baada ya kupata misaada wajiendeshe wenyewe,maana kuna muda miradi itakoma, ”alisema.
Safe akielezea mikakati ya kimenejimenti ya kukuza biashara ya taasisi husika hadi sasa wamefanya kazi na Benki ya Posta (TPB), Karagwe Development and Conservation Agency (KARUDECA),Tanzania Association of Micro Finance Institutions (TAMFI),SELF Microfinance Fund na Tume ya Ushirika Tanzania.
“Taasisi hizo zimenufaika kwa kupata ujuzi na utalaamu wa fedha, weledi katika utendaji kazi zao, kuboresha familia maskini na kuanzisha miradi endelevu.Pamoja na kufanya kazi na taasisi hizo lengo kuu ni kuona namna gani tutawafikia wananchi wengi zaidi,”alisema Mkurugenzi huyo Mkaazi wa SBFIC.
Hata hivyo alieleza zaidi kuwa mazungumzo baina ya serikali na SBFCI yanaendelea ili kuona jinsi gani watafanya mafunzo hayo na yakiwa tayari wataanzisha kufundisha elimu kwa vitendo hususani taasisi ndogo ndogo za kifedha.
Akifungua ofisi za SBFIC Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba ya Tubingen ya Ujerumani, Dr. Christoph Gogler alisema watatoa elimu kwa taasisi za kifedha nchini na kujenga uwezo wa wananchi kutokana na kubobea  kwenye masuala ya fedha na kutumia utaalamu wao wa miaka 150.
Alieleza kuwa mbali na kufungua ofisi amekuja kuangalia miradi inayofanyika Tanzania hasa katika eneo la kifedha lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutunza akiba ambapo pia kuitaziwezesha taasisi za fedha na benki humu nchini kupiga hatua ya maendeleo na kujenga uchumi imara

No comments :

Post a Comment