Friday, November 16, 2018

GUNIA 17 ZA BANGI ZAKAMATWA PWANI -WANKYO


aa
………………
Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa, akionyesha kiasi cha bangi kati ya magunia ya bangi yaliyokamatwa. Picha na Mwamvua Mwinyi
………………..
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 
JESHI la polisi mkoani Pwani, limewakamata watu wawili (wanaume) wanaodaiwa kusafirisha bangi gunia 17 ndani ya gari lao lenye namba za usajili T. 819 CYQ aina ya prado. 
Kamanda wa polisi mkoani hapo (ACP), Wankyo Nyigesa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema kwamba ,majina ya watuhumiwa hao yanahifadhiwa ambapo wamewakamata baada ya kupokea taarifa fiche kutoka kwa wasamalia wema . 
Alieleza, walipokea taarifa hizo kuwa watu hao walikuwa wanasafirisha shehena hiyo ya bangi,wakipitia barabara ya Bagamoyo kuelekea Dar es salaam. 
Nyigesa alitoa onyo, kwa wale wanaofanya biashara hiyo, wanaotumia na kusafirisha kuacha mara moja kwani inasababisha athari kwa afya na kuharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa. 
“Kama nilivyotangulia kusema kwa siku za hivi karibuni, hakuna mhalifu ama wahalifu watakaofurukuta mkoani hapa, “
“Kila atakaebainika atakutana na operesheni TINDUA TINDUA ya uhalifu, hivyo ni vyema wakaacha uhalifu, kusafirisha magendo, bangi kutumia madawa ya kulevya kwani lazima ukikamatwa upate joto ya jiwe “alieleza Nyigesa. 
Kamanda huyo aliiomba jamii, wawatume popote na wamwite kokote na wakati wowote yeye ataitika, na wasisite kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu unapopangwa ili kukomesha uhalifu mkoani humo.

No comments :

Post a Comment