Kamishna wa Ustawi wa Jamii Nchini
Dkt. Naftali Ng’ondi akiwa na Kamishna Msaidizi Bw. Rabikila Mushi
(katikati) pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii Bi. Rehema Kombe wa mwanzo
kushoto na Irene Kombe Afisa Ustawi wa Jamii jiji la Arusha akiongea na
vyombo vya habari kuhusu maandalizi ya Siku ya Kimataifa ya Wazee
Duniani yatakayofanyika jijini Arusha tarehe 1/10/2018.
Na Mwandishi Wetu. Arusha.
Umoja wa Mataifa umetenga kila
tarehe 1 Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee kwa lengo la kutafakari
hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili ili kuweka mipango
thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima,
hadhi na kuthaminiwa utu wao.
Haya yamesemwa na Kamishna wa
Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi wakati wa wa kikao chake na
waandishi wa habari mjini Arusha ili kuifahamisha Jamii juu ya
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani.
Kamishina Ng’ondi amesema Itifaki
ya Haki za binadamu ya Afrika kwa watu wazee ya Umoja wa Afrika ya mwaka
2016 pamoja na mambo mengine, imesisitiza kuwa kila mmoja anayo haki ya
kufurahia haki na uhuru unaotambuliwa na itifaki hiyo bila vikwazo
vyovyote kama vile rangi, ukabila, jinsia, lugha, dini, siasa au wazo,
mali na utaifa au jamii yake mahali pa kuzaliwa au hali nyingine.
‘’Ni kwa mantiki hiyo basi
Kiongozi wa Dini Nchini Afrika ya Kusini Askofu Desmond Tutu aliwai
kusema kuwa, jinsi tunavyozeeka, haki zetu hazizeeki kwa hiyo ni wajibu
wetu kuhakikisha wazee wetu Nchini wanaishi maisha mazuri na
yakuheshimika’’. Alisema Dkt. Ng’ondi.
Kila mwaka Maadhimisho haya hubeba Kaulimbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka huu 2018, kaulimbiu inasema “Wazee ni Hazina ya Taifa: Tuenzi Juhudi za Kutetea Haki na Ustawi Wao’’. Kaulimbiu hii inahimiza Serikali na Jamii kwa ujumla kutambua na kuenzi jitihada za Wazee katika ujenzi wa Taifa letu.
Dkt. Ngondi alisisitiza kuwa sera
ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003 inahimiza kuwatambua wazee kama
rasilimali muhimu katika maendeleo yetu,kuwashirikisha wazee katika
maamuzi muhimu yanayowahusu wao na Taifa kwa ujumla na kuwashirikisha
katika uzalishaji mali na kuondoa umasikini miongoni mwao.
Aidha alisema Sera hiyo pia
inasisitiza kuboresha huduma zinazotolewa kwa wazee, kutoa ulinzi wa
kisheria kwa wazee kama kundi maalumu na kuwaelimisha vijana kuhusu
masuala ya uzee na kuzeeka na kuwajengea uwezo wa kufanya maandalizi ya
maisha kuelekea uzeeni.
Kamishna huyo alitoa wito kwa
jamii kuwa haina budi kuenzi na kudumisha mila na desturi nzuri za
kuwaenzi wazee kwa kutambua kuwa wazee ndio chanzo cha urithi wa
historia ya nchi, washauri wa familia na jamii, watu wenye hekima na
walezi katika Taifa.
Na pia Kamishna huyo ameitaka
jamii kuwa na wajibu wa kuwaondolea vikwazo wazee katika kupata huduma
za kijamii ikiwa ni pamoja na afya, matunzo na ulinzi katika kipindi
chote cha maisha yao.
Maadhimisho haya kwa mwaka 2018
yanafanyika Kitaifa katika Jiji la Arusha na Mgeni Rasmi katika
maadhimisho haya anatarajiwa kuwa Mzee wetu Ally Hassan Mwinyi, Rais
Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maadhimisho ya Siku ya Wazee
Duniani ni moja ya jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN)
katika kutambua na kuhamasisha Serikali za Nchi Wanachama na wadau
wengine kuweza kulinda na kutetea haki za Wazee duniani kote.
No comments :
Post a Comment