Saturday, September 29, 2018

RAIS MAGUFULI ATAJA SABABU ZA KUMNG’OA NAIBU WAZIRI, KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NJE


jpm-660x400
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. John Magufuli ametaja sababu za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba na kumhamisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda.
Akizungumza katika hafla ya kumuapisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk.Damas Ndumbaro  iliyofanyika leo tarehe 29 Septemba 2018 Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema baadhi ya watendaji wa wizara hiyo hasa wakurugenzi wamekuwa wanafanya kazi kwa mazoea.
Dkt. Magufuli ameeleza kuwa, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akiwa nje ya nchi kikazi, baadhi ya wakurugenzi wamekuwa na tabia ya kumuendesha Naibu Waziri na Katibu Mkuu kutokana na viongozi hao kukosa msimamo.

“Kuna mikutano mingi Waziri atakuwa anatumwa na hata wewe, waziri muda mwingi anakuwa nje ya Tanzania ndiyo maana kuna naibu waziri, waziri akiwa hayupo naibu anakuwa msimamizi wa mambo yote, siyo naibu waziri kuendeshwa na wakurugenzi, na ndio maana nikaona nimtoe naibu waziri na katibu mkuu, nazungumza kwa uwazi bila kuficha,” amesema na kuongeza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemtaka Dkt. Ndumbaro kufanya kazi huku akimuagiza kuwa, kama atabaini kuna mtendaji au mkurugenzi mzigo asiyetekeleza vizuri majukumu yake kumuondoa kazini.

Aidha, amewataka watumishi wa wizara hiyo kutoa ushirikiano kwa Dkt. Ndumbaro katika utekelezaji wa majukumu yake.

No comments :

Post a Comment