Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza wakati
wa ziara yake aliyoifanya huko Msomngola ili kukagua eneo lililotakiwa litolewe
kama viwanja kwa wakazi waliopisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam Septemba 17, 2018.
NA
MWANDISHI WA TAA
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Richard Mayongela(kulia)
akifafanua jambo kwa wananchi wa maeneo ya Msongola, Ilala, Dar es
Salaam wanaodai malipo ya maeneo yao kwa Kampuni ya Tanzania Remix ili
yaweze
kugawiwa kwa wananchi waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa
Mwalimu Julius Nyerere. Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (kushoto) akisikiliza kwa makini
Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia)
akimsikiliza mmoja wa wananchi wenye mashamba eneo la Msongola, Ilala, Dar es
Salaam, Mrisho Kawete (wa kwanza kushoto) ambao hawajalipwa na Kampuni ya
Tanzania Remix iliyochukua mashamba yao kwa ajili ya kuwapatia wananchi
waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Mwakilishi
wa kampuni ya Tanzania Remix akitoa maelezo kuhusu viwanja 537 wanavyotakiwa
kuwapatia wananchi waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius
Nyerere.
Mhandisi Nditiye (kulia), akisikiliza malalamiko ya mmoja wa wananchi wanmaopaswa kufidiwa.(PICHA ZOTE NA MOHAMMED KIMWERI WA K-VIS BLOG)
NAIBU
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameielekeza
Mamlaka ya Viwanja va Ndege Tanzania (TAA) kufuatilia na kupata viwanja vyake 537
kutoka kwa kampuni ya Tanzania Remix kama makubaliano ya mkataba yalivyo kwa
ajili ya kuwapatia wananchi waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA)
Nditiye
ameyasema hayo katika ziara yake ya kukagua viwanja 537 kwenye eneo la Msongola
lililopo wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ambapo kampuni ya Tanzania Remix ilipewa jukumu na TAA ya kuandaa viwanja hivyo
takribani miaka mitano sasa ili viweze kugawiwa kwa wananchi waishio maeneo ya
Kipunguni A na Kipunguni Mashariki, Dar es Salaam waliopisha upanuzi wa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam kwa nia njema ili Serikali iweze
kuendeleza na kupanua uwanja huo.
Nditiye
amesema kuwa atafika tena kwenye eneo hilo baada ya wiki moja kukagua hatua
iliyofikiwa ya upatikanaji wa viwanja hivyo kwa kuwa jambo hilo limechukua muda
mrefu na Serikali haiko tayari kuona jambo hilo likiendelea pasipo kufika mwafaka
kwa kuwa lina sura ya ujanja ujanja na uongo uongo ambao hauko wazi ambapo wananchi wasio na hatia wanaumia bila sababu
Amefafanua
kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TAA imeilipa Kampuni
ya Tanzania Remix kiasi cha shilingi bilioni 3.7 ili waweze kuandaa viwanja
ambavyo vitakabidhiwa kwa wananchi hao waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa
JNIA. “Tumetembelea eneo hilo, tumejionee wenyewe, mmesikia wananchi wakiwa
wanalalamika kuwa Tanzania Remix hawajawalipa wananchi mashamba yao ili yapimwe
viwanja na kugawiwa wananchi waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa JNIA. TAA
wana mkataba kati yao na Tanzania Remix na ninaamini TAA wamewavumilia sana
Tanzania Remix. Nadhani sasa ni wakati TAA washikilie mkataba unasemaje na
muanze kuchukua hatua kwa kuwa jambo hili limechukuwa muda mrefu, wananchi wako
tayari kuachia viwanja na kupokea viwanja, hatuwezi kuona wananchi wananyanyaswa,”
Nditiye amesema.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bwana Richard
Mayongela amesema kuwa hadi hivi sasa kampuni ya Tanzania Remix imegawa viwanja
58 tu kwa wananchi kati ya viwanja 537 vinavyohitajika kugawiwa kwa wananchi na
kazi hiyo imechukua muda mrefu kukamilika na hivyo wanaichonganisha Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi walioridhia na kupisha upanuzi wa
uwanja wa ndege wa JNIA kwa nia njema. Mayongela amewaomba wananchi waendelee
kuwapa ushirikiano na kuvumilia jambo hili ili liweze kufanyiwa kazi na hakuna
haki ya mwananchi yeyote itakayopotea kwa kuwa wananchi kwa uzalendo wao
wamepisha eneo husika ili waweze kuona maendeleo ya taifa lao. “Mkataba huu ulikuwa
ni wa miaka miwili ila bahati mbaya huu ni wa mwaka wa nne au wa tano unaenda
na mkataba umeisha muda wake japo sisi tulilipa pesa nao watupe viwanja.
Nimeelekeza wanasheria wapitie mkataba husika na kama utakuwa haujatekelezwa,
TAA na wananchi tutachukua hatua ya kudai kampuni ya Tanzania Remix, hatutaki
kesi na wananchi hawatak kesi ila wanataka haki yako,” amesema Mayongela.
Akiwa
ziarani humo, Nditiye amezungumza na baadhi ya wananchi ambao maeneo yao ya
Msongola yametwaliwa na Kampuni ya
Tanzania Remix ili yaweze kuchukuliwa, kupimwa, kuwekwa miundombinu mbali mbali
na kugawiwa kwa wananchi waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa JNIA .
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake mbele ya Mhandisi Nditiye, Bwana
Mrisho Kawete amesema kuwa kampuni hiyo haijakamilisha malipo yote kwa wananchi
hao hivyo hawako tayari kwa maeneo yao kuchukuliwa na kupatiwa wananchi
waliopisha upanuzi. Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Luhanga, Kata ya
Msongola iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam Bwana Lwembu Henjewele amesema
kuwa wananchi wanaunga mkono jitihada za Serikali za kupanua uwanja huo na
wameridhia maeneo yao wapatiwe wananchi wanaohitajika kulipwa fidia ila tu
kampuni ya Tanzania Remix ikamilishe malipo kwa wananchi wake.
No comments :
Post a Comment