Monday, September 10, 2018

Miliki nyumba za gharama nafuu za makaazi Mbweni Zanzibar



                                               Baadhi ya nyumba za makazi Mbweni

Na Christian Gaya
Hadi sasa Tanzania ina mahitaji ya zaidi ya nyumba 3,000,000 (milioni tatu) kwa ajili ya makazi ya watu katika maeneo mbalimbali ya nchi. Na karibu asilimia kati ya 70 na 75 ya wananchi wa Tanzania wanaishi katika makazi holela.  

Kwa ajili ya kusaidia serikali katika kutatua changamoto zinazolikumba taifa mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) umeanza tayari kutekeleza sera yake ya uwekezaji wa kuhakikisha ya kuwa inafikia ukomo wake wa uwekezaji wa kufikia angalau asilimia ya 35 ya fedha za uwekezaji kila mwaka wa fedha zinatengwa kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo na hasa kwenye nyumba za gharama nafuu. 

Ambapo asilimia inayobakia inatumika kuwekeza kwenye dhamana za kiserikali, akiba ya muda maalumu, hisa kwenye makampuni, mikopo kwa makampuni, dhamana za makampuni na hisa kwenye soko la mtaji

 “Tumeamua kwanza kuweka mikakati zaidi kwa kuanza kujenga nyumba za gharama nafuu kwa watu wa kipato cha chini na wa kipato cha kati. Lengo letu ni kuhakikisha ya kuwa wateja wetu wanamiliki nyumba zao za kisasa zinazouzwa kwa bei nafuu ili kumwezesha kila mwanachama mchangiaji wa mfuko huu wa ZSSF na kwa Mtanzania yeyote anamiliki nyumba na kuboresha maisha yake” Sabra Machano ambaye ndiye mkurugenzi mwendeshaji wa ZSSF anasema.

Machano anasema ZSSF imepanga muda wa kumaliza wa kujenga mradi wa nyumba za gharama na nafuu zipatazo 140 kama jitihada za mfuko huo katika kujenga nyumba zenye staha kwa watanzania. Anasema mpaka sasa nyumba za Makazi Mbweni zipatazo 70 zimesha kamilika tayari mfuko umeanza kuziuza na awamu za awamu ya pili zinaendelea kujengwa. Nyumba hizi za watu wa kipato cha chini na cha kati zimelengwa kuuziwa wanachama wa ZSSF na mtu mwingine yeyote kwa mkopo wa muda mrefu.
Kulingana na maelezo yake Machano anasema mradi huu umepangiwa kutekelezwa kwa awamu kuu mbili, wakati awamu ya kwanza imekwisha tayari kwa kujenga nyumba zipatazo 70. Na awamu ya pili inategemewa kumalizika mnamo mwaka unafuata wa mwaka 2019 ambapo nyumba zitapato 70 zitakuwa zimesha jengwa tayari kwa mauzo kwa wanachama wa mfuko wa ZSSF na kwa mtu yeyote atakayetaka kununua.

Mtu yeyote anayehitaji nyumba za ZSSF Mbweni anaweza kununua kwa njia moja kati ya hizi tatu zifuatazo:- Kununua kwa fedha taslimu, Kununua kwa njia ya kupitia benki, Kununua kwa njia ya kukodi na kumiliki kwa muda wa miaka 15.
 
Baadhi ya nyumba za makazi Mbweni
 
“Nyumba hizo zilizokwisha malizika kujengwa za ZSSF Mbweni zinauzwa kuanzia shillingi milioni 168.82 za Kitanzania kwa vyumba viwili, shilingi milioni 190.84 nyumba yenye vyumba vitatu na shilingi milioni 249.56 kwa nyumba yenye vyumba vine, na mfuko umeanza tayari kupokea fedha hizo kuanzia sasa hata kwa mtu yeyote au wanachama yeyote anayetaka kutanguliza malipo kwa ajili hata zile zinaendelea kujengwa” anasema.

Sabra anawahakikishia kwa yeyote anayeweza kununua au kuwa mkazi wa ZSSF Mbweni, ya kuwa karibu atapata huduma zote za muhimu za kijamii zikiwemo shule na vyuo, hospitali, nyumba za ibada, sehemu za kupaki magari, sehemu za burudani na starehe na vifaa vyote vya usalama na ulinzi, sehemu za kuogelea, maduka kwa ajili vitu muhimu. 

Sabra Machano Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar


Anasema uwekezaji unafanywa kwa kuzingatia na kufuata kanuni za usalama wa mtaji, uwezo wa kuleta faida, uwezo wa kitega uchumi kubadilika kuwa fedha taslimu, kuchangia masuala ya kijamii, na kutawanya uwekezaji ambayo ndiyo misingi mikuu. Kwa kuzingatia kanuni ZSSF inawekekeza katika maeneo tofauti kwa viwango tofauti kulingana na sera ya uwekezaji kama vile kwenye dhamana za kiserikali, akiba ya muda maalumu, miradi ya ujenzi, hisa kwenye makampuni, mikopo kwa makampuni, dhamana za makampuni na hisa kwenye soko la mtaji. 

Miradi mingine ya ujenzi iliyotekelezwa na ZSSF ndani ya miaka 20 ni pamoja na mradi wa Pemba Conference Centre, mradi wa ZSSF Mwanakwerekwe Shopping Centre, Viwanja vya kufurahishia watoto vya Umoja Tibirinzi Pemba na Uhuru Kariakoo Unguja, 50 Anniversary Mapinduzi Tower –Michenzani, Ukarabati wa Jumba la Treni Darajani, Nyumba za Makaazi Mbweni 

Na miradi inayoendelea na iliyoanza ni pamoja na Nyumba za Makazi Mbweni, ZSSF Michenzani Mall –Michenzani, Zanzibar New City Kwahani. Miradi mengine ambayo inatarajiwa kutekelezwa na ZSSF ni pamoja na Kisonge Commercial Centre, Mombasa Affordable Housing Project, na Tunguu Affordable Housing Project

Anasema changamoto zinazoukabili Mfuko ni kuwa na faida ndogo ya uwekezaji hasa katika majengo, uwelewa mdogo wa sheria ya Mfuko, wigo mdogo wa wanachama kutoka sekta isiyo rasmi, ugumu wa ukusanyaji wa michango kutoka sekta isiyo rasmi, ugumu wa kuwasajili wafanyabiashara wadogo wadogo ambao kundi kubwa liko katika sekta isiyo rasmi na nyingine zikiwa ni uwelewa mdogo miongoni mwa wananchi juu ya dhana na sekta ya hifadhi ya jamii na, madai ya marejesho ya michango kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ambao ajira zao ni za mikataba ya muda mfupi. Aidha madai hayo hutokea pia kwa wafanyakazi wa Taasisi za Serikali wanaoachishwa kazi kabla ya kufikia umri wa kustaafu

Mipango ya baadae ya ZSSF ni pamoja na kuzijumuisha idara maalum za SMZ ili askari na maafisa wa idara hizo kuwa wanachama wa ZSSF na kupata mafao yao kupitia Mfuko huu, kuanzisha mafao kadhaa ya muda mfupi ikiwemo msaada wa mazishi kwa wanachama, kutanua wigo wa ofisi za ZSSF katika Mikoa na Wilaya mbalimbali ikiwemo kufungua ofisi ndogo Dar es Salaam.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment