Mmoja
wa wakurugenzi wa taasisi ya Friedkin Conservation Fund,(FCF) Abdukadir
Mohammed akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (katikati) Anthony Mtaka
akipokea hundi ya shilingi 110 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya
sekondari ya vipaji maalum Mkoa wa Simiyu jana katika viwanja vya
Maonesho ya Kilimo na Mifugo, Nyakabindi Mkoa wa Simiyu.
|
Mwandishi Wetu
TAASISI ya
uhifadhi na Utalii ya Friedkin Conservation Fund, imetoa msaada ya
shilingi milioni 110 ili kusaidia ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Vipaji
maalum mkoani Simiyu. Msaada huo, ulikabidhiwa jana kwa Mkuu wa Mkoa
wa Simiyu, Bw. Anthony Mtaka na wakurugenzi wa taasisi hiyo wakiongozwa
na Abdukadir Mohamed katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Maonesho ya
Nanenane Nyakabindi Wilaya ya Bariadi.
Mohammad
alisema taasisi yao ambayo inamiliki kampuni za Uwindaji na upigaji
picha za kitalii, Mwiba Holdings Ltd na Tanzania Game Trackers Safaris,
ambazo zimewekeza mkoani humo, zimetoa msaada huo kusaidia watoto kupata
elimu.
Alisema msaada huo ni mwendelezo wa misaada ya kusaidia jamii inayotolewa ili kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Simiyu kiujumla.
"Tunachoomba
ni kupewa ushirikiano tufanye kazi zetu za utalii katika pori la akiba
la Makao na Maswa na kuondolewa uvamizi," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alishukuru kwa msaada huo wa shilingi milioni 110 ambazo zitasaidia ujenzi wa shule hiyo.
Alisema
Taasisi ya Friedkin imekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo katika mkoa
huo kwani hivi karibuni ilitoa msaada wa mifuko 3000 ya saruji na bati
1000 kusaidia elimu pia.
Kulikuwepo
na migogoro katika eneo la mwekezaji huyo hivyo kabla ya kupokea
misaada ya Saruji na bati Mkuu huyo wa mkoa aliongea na Rais Dk. John
Mafuguli kuomba idhini ya kupokea.
"Niliona
ningepokea mwenyewe maneno yangeanza ya kuchafuana, hivyo niliomba
ridhaa ya Rais na akasema hii ni michango ya maendeleo tupokee. Mh. Rais
alisema na shule ikijengwa wanaweza hata kuiita Mwiba," alisema.
Alisema licha ya msaada huo, taasisi hiyo imesaidia kutoa mchango wa ajira na imekuwa ikilipa kodi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dk. Joseph Chilongani alisema
Serikali inatambua mchango wa taasisi hiyo kwa maendeleo ya jamii.
Alisema
licha ya misaada inayotolewa ngazi ya mkoa, taasisi hiyo kila mwaka
inatoa zaidi ya shilingi milioni 610 kama kodi ya pango na sehemu ya
mapato ya utalii kwa vijiji 10 vilivyopo eneo la hifadhi ya jamii ya
makao.
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mkoa wa Simiyu, Gungu Silanga alisema
Serikali ya CCM itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwani inachangia
utekelezwaji wa Ilani ya uchaguzi.
"Miaka
ya nyuma kulikuwa na watu wachache walitaka kutugombanisha lakini sasa
chama na Serikali tupo pamoja kufanya kazi na wawekezaji Mkoa wa
Simiyu,” alisema.
No comments :
Post a Comment