Wednesday, August 1, 2018

Sabuni za mwani zafika soko la Ulaya

PichaKhatib Suleiman, Zanzibar
MAFANIKIO ya wajasiriamali katika kusarifu matumizi ya bidhaa zinazotokana na mwani, yamewawezesha sasa kutengeneza sabuni za mwani na kuingia katoka soko la Ulaya.
Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali amesema hayo wakati akizungumza na
wajasiriamali wanaotengeneza bidhaa mbalimbali kuhusu mikakati ya kutangaza bidhaa zao kwa njia ya mtandao.
Balozi Amina amesema, bidhaa zinazotokana na sabuni ya mwani sasa ni maarufu katika nchi za Scandinavia ikiwemo Sweden.
Amesema hayo ni mafanikio makubwa yanayohitaji kuungwa mkono na Serikali katika kuona wajasiriamali wanapiga hatua kubwa ya maendeleo katika biashara zao.
''Nimefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na wajasiriamali mbalimbali katika kutengeneza bidhaa ambazo zimefanikiwa kuingia katika soko la nchi za Ulaya ikiwemo Sweden,'' alisema.
Alisema kazi kubwa inayofanywa na wizara kwa sasa ni kushajihisha wawekezaji, kuwekeza katika viwanda ambavyo vitasarifu bidhaa zinazotokana na mwani.
Mjasiriamali Khadija Kona alisema wanatengeneza sabuni zinazotokana na bidhaa ya mwani, ambazo zimepata soko kutokana na ubora wake ikiwemo wa kutibu maradhi mbali mbali ya ngozi.
Alisema bado wanahitaji ujuzi na mbinu zaidi katika utengenezaji wa bidhaa hizo ili kuingia katika ushindani wa soko la kimataifa.

No comments :

Post a Comment