Wednesday, August 1, 2018

MKULIMA WA MAHINDI AIOMBA SERIKALI IMSAIDIE KUOKOA TANI 7,200 ZA MAHINDI ALIYOVUNA BAADA YA KUKOSA SOKO


 Mahindi yaliyohifadhiwa nje ya maghala baada ya maghala hayo kujaa.
NA MWANDISHI WETU, RUKWA
 Mkurugenzi wa shamba la Msipazi lililopo katiika kijiji cha China, kata ya Kate, wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa, Bw. Salum Summry ameiomba serikali kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa kuona uwezekano wa kumtafutia soko la mahindi aliyovuna mwaka jana (2017) na mwaka huu (2018) ili kujiendeleza kibiashara.
Summry alisema kuwa tani 7,200 za mahindi yaliyopo yamejaza maghala na hatimae mahindi yanayoendelea kuvunwa huwekwa nje jambo ambalo litahatarisha usalama wa mahindi hayo endapo mvua zitaanza kunyesha mwaka huu.
“Tunaiomba NFRA iweze kununua tani zaidi za mahindi maana yake mwaka huu wamenunu tani 5,200 tu, tunaomba kutafutiwa soko, sisi peke yetu tuna tani 7,200 kwenye maghala yetu na mengine tunaendelea kuvuna na kuyahifadhi hapo uwanjani kutokana na upungufu wa ma-godown (maghala), na mpaka sasa gunia 250 zimeharibika ila tutazigeuza kuwa pumba, hivyo hatutapata faida wala hasara,” Alisema.
Summry amesema kuwa wameona umuhimu wa kujaribu kupanda zao la alizeti katika ekari 1000 ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya Mkoa katika kuliimarisha zao hilo huku ekari 3200 akiwa amepanda mahindi.
Ametoa maombi hayo alipotembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ikiongozwa na Mkuu wa mkoa Mh. Joachim Wangabo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo na kamati yake ya Ulinzi ili kuona maendeleo ya mwekezaji huyo na kuona namna ya kufikisha huduma muhimu katika eneo hilo ambalo linatariwa kujengwa kiwanda cha mafuta ya alizeti, chakula cha kuku, pamoja na unga.
Mh. Wangabo alisema kuwa serikali ipo pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha uchumi wa viwanda unafikiwa kwa asilimia 100 na kamwe haitawaangushga wawekezaji hao na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda kuwa karibu na mwekezaji huyo ili kuwezesha kusaidia kutimiza ahadi ya viwanda 100 kwa kila Mkoa.
“Nimeona kuna mlundikano mkubwa wa mahindi ya mwaka jana na mwaka huu, serikali ipo pamoja nawe katika kuhakikisha tunakupunguzia haya machungu, hivi karibuni Rais wetu alizungumza na shirika la WFP na wao wamesema kuwa wataongeza idadi ya kununua mahindi zaidi kutoka Tanzania, hivyo wasiliana na WFP kupitia NFRA ili nuwe wakala na kujihakikishia soko, lazima ujisajili nili uweze kuwasaidia na wakulima wengine kupata soko.”Alisema.
Pia Mh. Wangabo alitoa pongezi kwa mwekezaji huyo kwa kuunga mkono juhudi za mkoa katika kufufua zao la alizeti na kujenga bkiwanda cha mafuta hayo na kumuhakikishia kuwa kiwanda hicho kitapata malighali ya kutosha kutoka kwa wakulima wengine mkoani humo. 

 Mkurugenzi wa Shamba la Msipazi Salum Summry (kushoto) akifafanua jambo wakati akielezea umahiri wa mashine ya upandaji mbegu, mbele ya ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 
 Mkurugenzi wa Shamba la Msipazi Salum Summry (kushoto) akifafanua jambo wakati akielezea umahiri wa mashine ya upandaji mbegu, mbele ya ya mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 
 Mkurugenzi wa Shamba la Msipazi Salum Summry (kushoto) akitoa maelezo ya mashine ya kumwagia dawa katika ekari 320 kwa siku. 

 Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiangalia uvunaji wa kisasa katika shamba la mahindi la msipazi. 
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akijaribu kuendesha gari ya kuvuna mahindi yenye uwezo wa kuvuna Zaidi ya ekari 90 kwa siku.

No comments :

Post a Comment