Wednesday, July 11, 2018

TDB yatoa bil 900/- ujenzi wa SGR

PichaMwandishi Maalumu
BENKI ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), itaikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 400 sawa na takriban Sh bilioni 900, kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha
umeme wa gesi wa Kilwa.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na rais wa benki hiyo yenye makao yake makuu jijini Nairobi, Kenya, Admassu Tadesse, alipokutana na kufanya mazungunzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani. Tadesse alisema kuwa benki yake imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati ya kisasa pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa mkoani Lindi.
“Tanzania ni mdau mkubwa wa benki hii ikiwa inashika nafasi ya 7 kati ya nchi na taasisi 37 zinazomiliki hisa zake ambapo inamiliki hisa asilimia 6.4,” alisema Tadesse. Alisema kuwa hadi Machi, mwaka huu, benki yake inatekeleza miradi 11 ya maendeleo nchini Tanzania, katika Sekta ya Kilimo, Biashara, Huduma za Benki na Fedha, Nishati, Ukuzaji Miundombinu na Viwanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni.284.6 “Tuna miradi mingine iliyoidhinishwa na Benki, inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 157 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 660 ambacho kimepangwa kutolewa kwa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kilimobiashara, ujenzi, kemikali na petroli pamoja na sekta ya nishati,” aliongeza Adesse.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujiimarisha kimtaji na kiuendeshaji na kwamba Tanzania inapokea kwa mikono miwili ahadi ya benki hiyo ya kushiriki katika ujenzi wa miradi ya kipaumbele ya Taifa, ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na Mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa, itakayochochea uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dk Kalemani alisema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa, utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 318 na utaongeza kiwango cha upatikanaji umeme nchini ambacho hivi sasa kimefikia megawati 1,500. TDB inaundwa na nchi 22 za Kiafrika, nchi mbili ambazo si nchi za Kiafrika pamoja na taasisi za uwekezaji 13 na kufanya idadi ya nchi na taasisi ambazo ni wana hisa, zinazounda benki hiyo, kufikia 37.

No comments :

Post a Comment