Thursday, July 19, 2018

Mbowe, wenzake kuisubiri Makahama Kuu

PichaFrancisca Emmanuel
KESI ya kufanya mkusanyiko usio halali na uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo Mwenyekiti wake Freeman Mbowe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeahirishwa hadi Julai 25, mwaka huu kwa ajili ya kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu.

Wakili Mkuu wa serikali, Faraja Nchimbi leo amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo imepelekwa kwa ajili ya kutajwa ili kusubiri uamuzi wa maombi yaliyopelekwa Mahakama Kuu.
Nchimbi akisaidiana na Wakili Zainabu Mango na Saimon Wankyo, amedai kuwa maombi ya awali yalisikilizwa wiki iliyopita na kwamba imepangwa kesho kwa ajili ya kutolewa maamuzi, hivyo wanaomba ipangwe tarehe ya karibu kwa ajili ya kusubiri uamuzi utakaotolewa.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai kuwa, mapingamizi ya awali yameshatolewa na upande wa mashitaka, hivyo wanaomba mahakama iendelee kuitaja kesi hiyo kutegemea Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi.
Amedai kama mapingamizi hayo yatafanikiwa basi kesi itapangwa kwa ajili ya kusikiliza na kama hayatafanikiwa itaendelea kupangwa kwa ajili ya kutajwa.
Viongozi hao waliwasilisha maombi Mahakama Kuu kuomba ipitie mwenendo wa kesi inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, mshitakiwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuuguliwa na mke wake ambaye amelazwa katika hospitali ya Bugando na mdhamini kuleta vithibitisho hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 25, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Mbali na Mbowe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Pia wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 12, ambapo wanadaiwa kuwa walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu katika maeneo ya Viwanja vya Buibui, Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni.
Wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washitakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kusababisha uvunjifu wa amani.
Inadaiwa kitendo cha kugoma kulisababisha hofu iliyochangia kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline na majeruhi kwa askari wawili ambao ni H.7856 PC Fikiri na E.6976 CPL Rahim Msangi.

No comments :

Post a Comment