Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kushoto akibadilishana mawazo na Balozi wa
Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi (kulia) mara baada ya
kumalizika kwa mkutano wa uwekezaji kati ya Shirika la Fedha la
Kimataifa-IMF na Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini Washington DC
Marekani, katikati ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo Bw. John
Rubuga.
Balozi wa Tanzania nchini
Marekani Mhe. Wilson Masilingi (kulia) akifafanua jambo kwa Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga (katikati) na Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere, wakati wa mkutano
Benki ya Dunia na IMF wa majira ya Kipupwe, mjini Washington DC,
Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) na Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Prof. Florens Luoga (kushoto) wakifuatilia kwa makini
majadiliano kuhusu uwekezaji ambayo yamejumuisha nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwemo Mawaziri wa Fedha na Magavana wa
Benki Kuu, mjini Washington DC Marekani.
Majadiliano yakiendelea kuhusu
namna Serikali zinavyoweza kushirikiana na Sekta Binafsi ili wapate
mikopo katika taasisi za fedha ili kukuza uwekezaji na biashara kwa
ujumla, majadiliano yaliyofanyika wakati wa moja ya mikutano ya Benki ya
Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF inayoendelea mjini
Washington DC, Marekani.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kulia akibadilishana mawazo na Gavana wa
Benki Kuu Mstaafu Prof. Benno Ndulu (kushoto) walipokutana katika
mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la
Kimataifa-IMF inayoendelea mjini Washington DC, Marekani.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)
…………………………………………………………………………..
Na. Mwandishi wetu- Washington D.C
Sekta binafsi inatakiwa
kuhakikisha fedha inazokopa kwa ajili ya uwekezaji au biashara
zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili waweze kurejesha mikopo yao
kwa wakati na
hivyo kupunguza ongezeko la Mikopo Chechefu (NPL).
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) aliyasema hayo wakati wa mkutano wa
uwekezaji uliojumuisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
ulioangazia changamoto ya upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi kutoka
taasisi za fedha katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, katika mikutano
ya kipupwe inayoendelea mjini Washngton DC, Marekani.
Amesema kuwa, licha ya kuwepo kwa
wakopaji wasiorejesha mikopo kwa wakati pia mwenendo mzima wa baadhi ya
taasisi za fedha zikiwemo benki kutozingatia kanuni na taratibu za
ukopeshaji, jambo linalosababisha kuongezeka kwa mikopo chechefu.
Akizungumzia kuhusu kupungua kwa
mikopo kwenye Sekta binafsi katika Jumuiya hiyo, Waziri Mpango amewataka
wananchi watambue kuwa ziko changamoto ambazo zinatokana na mahusiano
ya kiuchumi ya ulimwengu yanayosababisha kupungua kwa bidhaa ambazo
zinauzwa nje ya nchi hivyo kuathiri sekta binafsi.
Amesema matokeo kupungua kwa
biashara ama mauzo nje ya nchi kumewafanya wafanyabiashara kupunguza
uwezo wao wa kurejesha mikopo waliyokopa katika benki, hivyo wananchi
wasione kama ni tatizo la jumuiya hiyo tu bali lazima kuunganisha
kinachotokea na mwenendo wa kibiashara kimataifa.
Sababu nyingine ni kupungua kwa
fedha zilizokuwa zinaingia katika mfumo wa kibajeti miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka kwa nchi wahisani na hivyo kuzifanya
nchi kukopa kwenye taasisi za fedha za ndani ili kutekeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo.
“ Katika majadiliano haya
tumekubaliana kuendelea kuzungumza na sekta binafsi na kushughulikia
matatizo yanayowakumba hasa suala la malipo ya madai yao mbalimbali ili
waweze kulipwa haraka na kuondoa vikwazo katika mitaji yao ya biashara
ili waweze kurejesha mikopo waliyokopa katika benki.” alisema Dkt.
Mpango.
Kwa upande wake Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, ambaye alishiriki
majadiliano hayo ya uwekezaji alisema kuwa, sekta binafsi ina umuhimu
mkubwa katika kukuza maendeleo ya nchi kupitia uwekezaji wao.
“Nchi za Afrika Mashariki
zisipokuwa na uwekezaji mkubwa kupitia sekta binafsi, benki zitakosa
utayari wa kutoa mikopo kwa sekta hizo kwa kuwa na wasiwasi wa
urejeshwaji wa mikopo hiyo”, alieleza Gavana Luoga.
Amesema nchini Tanzania benki
binafsi zimeanza kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta binafsi, hata
hivyo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inafanya majadiliano na benki hizo ili
kuangalia jinsi zinavyoweza kuongeza uwekezaji kwa kutoa mikopo huku
jambo linalotakiwa kutiliwa mkazo ni ushirikiano na sekta hizo ili
ziweze kukopesheka suala ambalo Serikali imekuwa ikilijadili pia na nchi
nyingine na kuwa na mafanikio chanya.
Mkutano huo wa uwekezaji
uliojumuisha nchi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
ulihudhuliwa na Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za Afrika
Mashariki na kuwa na mafanikio makubwa kwa mstakabali wa maendeleo ya
jumuiya hiyo hasa katika Sekta ya Fedha.
No comments :
Post a Comment