Na Mwandishi Maalum
19/3/2018 Jumla ya wagonjwa 25
wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua katika kambi
maalum ya matibabu ya siku sita inayofanyika katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI).
Upasuaji huo unafanywa na
madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa
JKCI kwa
kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Open Heart International (OHI) ya
nchini Australia.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya upasuaji
Bashir Nyangasa alisema wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji watoto ni 15
na watu wazima 10.
Dkt. Nyangasa alisema kambi hiyo
imeenda sambamba na upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wagonjwa 65 kati ya
hao watoto 35 na watu wazima 30. Wagonjwa ambao wamefanyiwa uchunguzi
na hawatafanyiwa upasuaji katika kambi hiyo watafanyiwa upasuaji na
madaktari wa JKCI.
“Watoto tunaowafanyiwa upasuaji ni
wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na
mishipa ya damu kutopitisha damu vizuri katika moyo na kwa watu wazima
tunapandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass
Grafting) na kubadilisha milango ya moyo miwili hadi mitatu iliyoziba
au haifungi vizuri.
Kabla ya kuanza kwa kambi hiyo
kulikuwa na mafunzo ya kiuguzi ya siku tano ya utoaji huduma bora kwa
wagonjwa wa upasuaji wa moyo yalitolewa na Taasisi ya Open Heart
International kwa wauguzi 30 wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
Hadi sasa wagonjwa wanne
wameshafanyiwa upasuaji wa moyo kati ya hao watoto wawili na watu
wazima wawili na hali zao zinaendelea vizuri .
No comments :
Post a Comment