Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kidundai, Ndg. Waziri Mdoe (Kushoto) akipokea mfano wa hundi ya shilingi
milioni nne kutoka kwa mwakilishi wa TPDC, Ndg. Asiad Mrutu (Kulia).
Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya jengo la zahanati inayoendelea
kujengwa katika Kijiji hicho.
Na Mwandishi Wetu.
Katika jitihada endelevu za
utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji kwa jamii, Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) ambalo ni Shirika la Mafuta la Taifa kwa mujibu
wa Sheria ya Petroli (2015) limeendelea kuitekeleza dhana hiyo kwa
vitendo kwa kutoa vifaa vya
ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Kidunda
Wilayani Lushoto Mkoani Tanga.
Katika tukio hilo lililofanyika
mwishoni mwa wiki iliyopita, TPDC imeweza kukabidhi hundi ya Shilingi
milioni nne ambazo Kijiji kiliomba kusaidiwa ili kuwezesha ujenzi wa
zahanati hiyo ambapo kwa mujibu wa serikali ya Kijiji, fedha hizo
zitawezesha manunuzi ya mizunguko ya nondo 40 yenye futi 40 kila moja,
mifuko ya saruji, matofali na gharama za kumlipa fundi ambapo mpaka
kufikia hapo zahanati itakuwa imefanikiwa kuezekwa.
Akizungumza na mwandishi wa
habari mara baada ya kumaliza makabidhiano, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kidundai kilichopo Kata ya Vuga, Waziri Mdoe alisema “kwa niaba ya
halmashauri ya kijiji, tunayo furaha isiyo kifani kwa ndugu zetu kutoka
TPDC kwa moyo wa kutoa walioonyesha kwa kusaidia ujenzi wa zahanati yetu
ambayo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji hicho ili
kuondokana na adh ya kutembea umbali wa kilomita nane ili kupata huduma
ya afya”.
Mdoe aliongezea kuwa, ni
matumaini ya kijiji kwamba TPDC litaendelea kuwa mdau mkubwa wa
maendeleo katika Kijiji cha Kidundai kwani mahitaji yao ni mengi
yakiwemo maji, barabara na shule
Akikabidhi mfano wa hundi kwa
Mwenyekiti wa Kijiji kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Asiad
Mrutu ambaye ni Mjiolojia alisema “kipekee nimshukuru Mwenyekiti na
Wajumbe wa Serikali ya Kijiji kwa ushirikiano waliouonyesha toka
tulipofika siku ya kwanza katika Kijiji hiki tukiwa na lengo la kutafuta
eneo la uwekezaji, niseme tu kuwa huu ni mwanzo na tutaendelea
kushirikiana bega kwa bega kusukuma gurudumu la maendeleo ya Kidundai
mbele.”
Pamoja na kukabidhi hundi hiyo,
Mrutu aliusisitiza uongozi wa Kijiji kuchanganua gharama za miradi ya
maendeleo iliyopo katika mipango ili kurahisisha pale ambapo mdau wa
maendeleo anaetaka kuchangia kufahamu ni kiasi gani kitatosha badala ya
kueleza mahitaji kwa ujumla, hii itasaidia kupata msaada kirahisi na pia
kupata msaada unaokidhi mahitaji ya mradi husika.
Mchango wa ujenzi wa zahanati
hiyo umekuja baada ya TPDC kufanikisha zoezi la kupata ardhi kwa ajili
ya miradi ya kimkakati ya utafiti wa mafuta na gesi hapa nchini kwa
lengo la kuongeza kiasi cha gesi asilia nchini ambacho kwa sasa ni futi
za ujazo trilioni (TCF 57.538) na upatikanaji wa mafuta ili kuweza
kulihakikishia taifa nishati ya kutosha kwa ajili uzalishaji wa umeme,
vyombo vya usafiri, matumizi ya nyumba na kuhakikishia nishati ya
kutosha kwa maendeleo ya viwanda nchini.
No comments :
Post a Comment