Saturday, March 24, 2018

SERIKALI YATANGAZA KUTOA BINGO KWA WATAKAOSAIDIA KUWAFICHUA WEZI WA ALAMA ZA BARABARANI


a
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa(kushoto)  akisikiliza maelezo jana ya Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Damian Ndabalinze (wa pili kutoka kulia) mara baada ya kukagua kipande cha barabara Tabora hadi Nyahua kwa ajili ya kujionea wizi wa alama za barabarani na eneo lililokarabatiwa la Nyahua kutokana na uharibifu uliosababishwa na maji ya mvua ya kukata mawasiliano baina ya Itiga na Tabora.
b
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa( wa pili kushoto) alichungulia jana mkondo  wa maji katika eneo la Nyahua yaliyosababisha kipande barabara katika eneo la Nyahua wilayani Uyui kukatika na kusababisha mawasilano baina ya Tabora ya Itigi kukatika. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Damian Ndabalinze .
c
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa(kushoto)  akitoa maelekezo jana katika eneo la Nyahua wilayani Uyui  kwa Mwakilishi wa Kampuni ya CHICO  Peng Hao (kulia) mara baada ya kutembelea eneo la barabara ya Itigi hadi Tabora lililoharibiwa na maji ya mvua.
Picha na Tiganya Vincent
………………..
NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
SERIKALI imetangaza kutoa zawadi nomo kwa wananchi watakaosaidia kutoa taarifa za siri za kuwafichua watu wanaong’oa alama za barabarani na kuisababishia hasara kutokana na urejeshaji wake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Elias Kwandikwa  mara baada ya kukagua ukarabati wa eneo Nyahua ambalo lilikuwa limekatika kutokana na maji ya mvua yaliyopelekea kukosekana kwa mawasiliano baina ya Itigi na Tabora jana wilayani Uyui.
Alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuweka alama za barabara ili kuwaongoza watumiaji wa barabara kuepuka ajali lakini baadhi ya watu wamekuwa wakihuju na kung’oa alama hizo kwa ajili ya kwenda kuziua kama vyuma chakavu.
Kwandikwa alisema mtu atakayesaidia kutoa siri ya wanaong’oa alama hizo na wanunuzi wake atapewa zawadi na jina lake halitafichuliwa kwa ajili ya usalama wake.
Alisema inasikitisha kuona kuwa alama zipatazo 78 zenye thamani ya shilingi milioni 27 katika kipande cha barabara ya urefu kilometa zipatazo 80.6 kutoka Tabora hadi Nyahua zimeng’olewa.
Naibu Waziri huyo alisema alama hizo zinatumia fedha nyingi za Serikali kwa kuwa baadhi yake zinatoka nje ya nchi na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni hatari sana ni vema wahusika wakikamatwa washitakiwe kama wahujumu uchumi.
Alisema hata pale Serikali ilipoamua kujengwa alama hizo kwa Sementi bado baadhi ya watu wamekuwa wakizivunja ili kutoa nondo zilitumika katika ujenzi wake.
“Fikiria katika muda wa siku moja alama zaidi ya moja alama za barabarani 30 mkoani Kilimanjaro zimeng’olewa … Je? Kwa mwezi ni alama ngapi zinang’olewa ..pesa ngapi za Serikali inapotea kurudisha alama hizo …Ma RC na Ma DC na wananchi saidieni katika kupambana na wahujumu wa miundombinu katika maeneo yenu” alisema Kwandikwa.
Aidha Naibu Waziri huyo alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wauzaji na wanunuzi wa vyuma chakavu watakoa patikana na alama za barabara ili iwe fundisho kwa watu wanohujumu miundimbinu.
Kwandikwa alisema jamii inawajua vema wanaonunua vyuma chakavu ni vema wakatoa taarifa za siri ili kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa likichangia sehemu ya ajali nyingine za barabarani.
“Meneja wa TANROADS nafikiri tuanze kutoa kiasi fulani cha fedha kwa mtu anayetusaidia kutoa taarifa za siri kwa watu wanaong’oa alama za barabarani ili tukomesha tatizo” alisema Naibu Waziri.
Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tabora ilielezea kusikitishwa kwake na wizi wa alama za barabarani katika barabara nyingi za Mkoa huo na kuagiza viongozi wa maeneo husika ambapo barabara kuu zinapita wasimamie ulinzi.

No comments :

Post a Comment