Na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens
Luoga.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens
Luoga (wa pili kutoka kushoto), akiongoza kikao na watendaji wakuu wa
mabenki na taasisi za fedha kilichofanyika BoT makao makuu jijini Dar es
Salaam tarehe 23 Machi, 2018. Wengine kuanzia kushoto ni Manaibu
Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael, Dkt. Bernard Kibesse na Dkt. Yamungu
Kayandabila.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens
Luoga, amesema kipaumbele chake ni kukuza na kuendeleza ushirikiano kati
ya mabenki, Benki Kuu na Serikali.
Ameyasema hayo wakati alipoongoza kikao
chake cha kwanza na watendaji wakuu wa mabenki na taasisi za fedha
kilichofanyika BoT makao makuu jijini Dar es Salaam.
“Lengo langu kuu ni kukuza ushirikiano miongoni mwa
mabenki, Benki Kuu na Serikali,” alisema Prof. Luoga wakati akijibu
swali kutoka kwa mmoja wa washiriki wa mkutano huo aliyetaka kujua
vipaumbele vya Gavana huyo. Hiki ni kikao cha kwanza cha Prof. Luoga na
wakuu hao wa mabenki na taasisi za fedha tangu ashike madaraka ya
ugavana mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu.
Katika kikao hicho, Benki Kuu iliwaeleza wakuu hao wa
mabenki na taasisi za fedha hali ya uchumi ilivyo hapa nchini, kikanda
na duniani na mwelekeo wa utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi
kijacho kama ulivyopitishwa na Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania.
Baadhi ya wakuu wa mabenki na taasisi za fedha
katika kikao hicho.
Kushoto, washiriki wa Benki Kuu katika kikao hicho na
kulia, Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, akizungumza na
Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) na Mkurugenzi Mkuu wa
Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei, mwishoni mwa kikao hicho.
Katika kikao hicho viongozi hao wa sekta ya kifedha
hapa nchini walibadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya kibenki
na uchumi kwa ujumla.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki nchini (TBA),
Dkt. Charles Kimei, alimpongeza Gavana Luoga kwa kuanzisha utaratibu wa
kukutana na viongozi wa benki moja moja na akamuomba aweze kuandaa
mkutano kati ya BoT na TBA ili kujadilia masuala mbalimbali
yanayowahusu.
Kwa kawaida, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania hukutana
na wakuu wa mabenki na taasisi za fedha kila baada ya kikao cha Kamati
ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania na
wakati wowote atakapoona inafaa.
Kushoto, Prof. Florens Luoga akizungumza na Ofisa
Mtendaji Mkuu (CEO) wa Standard Chartered Bank Tanzania Ltd, Bw. Sanjay
Rugani, mwishoni mwa kikao huku Manaibu Gavana, Bw. Julian Banzi Raphael
na Dkt. Bernard Kibesse wakisikiliza. Kulia, Naibu Gavana Dkt. Kibesse
akizungumza na CEO wa International Commercial Bank (Tanzania) Ltd, Bw.
Ramakrishna Marakani, huku Gavana Luoga na Naibu Gavana Raphael
wakifuatilia mazungumzo hayo.
No comments :
Post a Comment