Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Kakunda akipanda juu ya
tanki la maji alipokagua mradi wa maji ya Ziwa Victoria wilayani
Kishapu alipofanya ziara hivi karibuni.
Mafundi wakiendelea na kazi ya
utandazaji mabomba katika mji wa Kishapu kwa jili ya usambazaji maji
kutoka mradi wa Ziwa Victoria unaoendelea kutekelezwa wilayani humo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa
mwaka 2017, Amour Hamad Amour akimtwisha ndoo ya maji mwanachi wa kata
ya Maganzo wilayani Kishapu ikiwa ni uzinduzi wa huduma hiyo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Mhe. George Kakunda (mwenye Kaunda katikati) akitoa maelekezo
kwa viongozi mbalimbali alipokuwa katika eneo Utemi kata ya Mwadui
Lohumbo palikojengwa toleo la kusambaza maji ya Ziwa Victoria kwenda
kwenye vijiji
……………………
Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi
Maji ni moja ya mahitaji na
rasilimali muhimu kwa uhai wa binadamu, wanyama na mimea ambapo
yanapatikana kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo vya asili na vya
kutengenezwa.
Katika Wilaya ya Kishapu Mkoa
wa Shinyanga vyanzo vikuu vya maji kwa wananchi wake ni
pamoja na visima
vifupi, virefu, mabwawa na miradi michache ya maji ya bomba.
Mahitaji halisi ya maji kwa
sasa katika wilaya hiyo ni mita za ujazo 15,303 kwa siku, lakini kiasi
cha mita za ujazo 7,860.7 tu ndizo zinazoweza kupatikana na kutumiwa na
wananchi wake.
Kutokana na na changamoto ya
uhaba mkubwa wa maji unaosababishwa na mvua inayonyesha kwa kiwango
kidogo kwa sasa wakazi wake wananufaika na huduma hii kwa kiwango cha
wastani wa asilimia 51.6 vijijini na asilimia 45 mjini.
Itakumbukwa kuwa kwa wastani
inakadiriwa kuwa Wilaya ya Kishapu hupata mvua inayonyesha kwa kiasi cha
milimita 450 hadi 900 kwa mwaka.
Hata hivyo, kwa kuzingatia
lengo la Taifa la kuwafikishia wananchi wa vijiji asilimia 90 ya maji
safi na salama ndani ya umbali wa mita 400 ya makazi yao ifikapo mwaka
2020, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kushirikisha Serikali Kuu,
wadau na wananchi imepunguza tatizo hilo.
Hivi karibuni ilianza kwa kasi
ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji kwa mradi wake wa maji ya Ziwa
Victoria ambao unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh. bilioni 1.16.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
hiyo, Stephen Magoiga anabainisha kuwa mradi huo ulianza mwishoni mwa
Oktoba mwaka huu baada ya taratibu za manunuzi ya bomba kukamilika
ambapo hadi sasa umefikia asilimia 80.
Kazi zilizofanyika na kukamilika
ni pamoja na uchimbaji mtaro wa kulaza bomba umbali wa mita 23,256
ambalo lina kipenyo cha milimita 315 na urefu wa mita 23,256 pamoja na
kuunganisha viungio mbalimbali vya bomba na ‘valve’ za kuondolea hewa.
Kwa mujibu wa Magoiga ni kwamba
hadi sasa takriban sh. milioni 820 kimetumika kununua mabomba, viungio,
dira za maji 1,500 pamoja na shughuli mbalimbali za mradi huo.
Bomba hilo limepitia katika
vijiji 16 ambavyo kwa sasa havina huduma ya maji na yanaweza kuhudumia
zaidi ya watu 45,000 hivyo Halmashauri inafanya jitihada za kutafuta
fedha za kuyasambaza.
Mradi huu ni mwendelezo wa upanuzi
wa mtandao wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika Mji wa Kishapu
kupitia Maganzo na Mgodi wa Almasi wa Mwadui.
Itakumbukwa ujenzi wa mfumo wa
usambazaji maji ulihusisha ulazaji wa bomba la maji lenye urefu wa
kilomita 70.2 kutoka Old Shinynga na ujenzi wa tangi la kuhifadhia maji
lenye mita za ujazo 1,200 mjini Kishapu.
Hivi sasa kwa wananchi wa wilaya
hiyo changamoto ya uhaba wa maji imeweza kutatuliwa kwa asilimia kubwa
hali inayoweza kuchangia kuendelea kuimarika kwa uchumi.
Kwa maji safi na salama
yanayopatikana kutoka chanzo cha Ziwa Victoria sasa wananchi wanaweza
kufanya shughuli za maendeleo tofauti na ilivyokuwa nyuma ambapo
walikuwa wakitumia muda mwingi kusaka maji.
Idara ya Maji katika Halmashauri
ya Wilaya Kishapu ikiongozwa na Mhandisi Lucas Said ambayo kwa sasa
imezaa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira inaendesha mradi huo.
Awali ilikuwa ikisambaza maji
kutoka chanzo kidogo cha maji kutoka Mto Tungu uliopo mjini Mhunze
ambapo hata hivyo huduma hiyo ilikabiliwa na changamoto ikiwemo
upungufu wa maji.
Kwa sasa baada ya kulifikisha
bomba la maji kutoka chanzo cha ziwa hilo huduma ya maji imekuwa ya
uhakika zaidi na saa za kufungulia maji zimeongezeka ikilinganishwa na
awali.
Tayari tangi la maji lenye ujazo
wa lita milioni 1.2 limekamilika ambapo hivi karibuni katika ziara yake,
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), George Kakunda alikagua mradi huo.
Akizungumza akiwa kwenye mradi huo
wa tanki la maji alipongeza juhudi za Halmashauri hiyo kwa kushirikiana
na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Kahama-Shinyanga (Kashwasa)
katika kuutekeleza.
Tanki hilo litakuwa likipokea maji
kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza katika Mji wa Mhunze na vitongoji
vyake na hivyo kuweza kutatua changamoto ya uhaba wa maji kama
ilivyokuwa awali.
Halmashauri hiyo iko katika
mikakati ya kuiomba Serikali Kuu kuisaidia fedha za kuzambaza maji hayo
katika Mji wa Kishapu na vijiji vingine pamoja na kufanya usanifu na
kujenga miundombinu ya majitaka.
Inaendeleza utafiti wa vyanzo
vingine zaidi vya maji na kuyatumia ya ziwa hilo kuyasambaza vijiji
vilivyopo jirani na bomba kuu. Pia kuelimisha jamii juu ya uchangiaji wa
gharama za ujenzi, uendeshaji na ukarabati wa miundo mbinu ya maji.
Aidha, utekelezaji wa Programu ya
Maji na Usafi wa Mazingira katika vijiji 10 ulianza kwa mchakato wa
kupata wataalamu washauri (consultants) wakisaidia kusanifu miradi,
kutafiti maji ya ardhini na kusimamia kuchimba visima virefu na baadaye
kuanza ujenzi wa miundombinu yake.
Programu hii ilijenga miradi
ya maji katika baadhi ya vijiji kadri fedha ilivyokuwa ikipatikana na
vilivyopewa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu kupitia awamu ya
kwanza ya utekelezaji vilikuwa tisa.
Vijiji hivyo ni Nyenze, Iboja,
Sekeididi, Mwigumbi, Mwamashimba, Bubinza, Mwamadulu, Idukilo na
Bunambiyu ambapo jumla ya Sh. bilioni 3.5 zimetumika kuitekeleza kwa
kuanzia usanifu hadi ujenzi wa miundombinu ya maji. Kwa pamoja miradi
hiyo inahudumia wananchi takriban 24,750.
Mkakati wa Halmashauri
Katika mpango na bajeti ya mwaka
wa fedha 2017/2018 Halmashauri iliidhinishiwa kiasi cha Sh. bilioni 1.6
kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira na hadi
kufikia Novemba imeshapokea Sh. milioni 26 ambazo ni kwa ajili ya
usanifu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi.
Utekelezaji wa Programu ya Maji
awamu ya pili umeanza katika mwaka huu wa fedha kwa kuhusisha jumla ya
miradi mitano katika vijiji vya Shagihilu, Ndoleleji, Lagana, Ikonongo
na Unyanyembe.
Aidha, wakandarasi wako eneo la kazi (site) wakiendelea
na ujenzi ambao uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na unaelezwa
kuwa unatarajia kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 1.5.
Halmashauri hiyo pia imeweza
kutekeleza mradi mwingine katika mji wa Maganzo ambao awali haukuwa na
huduma ya maji hivyo kusababisha wakazi takriban zaidi ya 12,000
kutokuwa na uhakika wa huduma ya maji safi na salama.
Mji huu umefanikiwa kupata maji
kutoka Ziwa Victoria kupitia ufadhili wa Shirika la Investing in
Children and their Society (ICS) kwa gharama ya Sh. milioni 750. Ujenzi
huo ulikamilika Machi 2017 na unahudumia wakazi wa Maganzo na kijiji cha
Masagala.
Hata hivyo changamoto
hazikosekani katika kutekeleza miradi ya maendeleo uhaba wa vyanzo vya
maji vya kutosha na vya kuaminika unakabili utekelezaji wa mradi huo.
Mkakati uliopo ni Kuendeleza
utafiti wa vyanzo vingine zaidi vya maji na kuyatumia maji ya ziwa
Victoria na kuyasambaza vijiji vilivyopo jirani na bomba kuu
Pia uhaba wa fedha kwa miradi ya
maji inayohitaji fedha nyingi unasababisha mradi kupata changamoto
katika utekelezaji wake na hivyo wananchi kukosa huduma hiyo muhimu.
Elimu inaendelea kutolewa kwa
jamii kuhusu ya uchangiaji wa gharama za ujenzi wa miradi hiyo na pia
uendeshaji na ukarabati wa miundombinu ya maji.
No comments :
Post a Comment