Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon
Sirro anawashukuru Wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa
Jeshi la Polisi jambo ambalo limesaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi
kikubwa hapa nchini. Kiujumla hali ya usalama hapa nchini ni shwari na
matukio makubwa ya uhalifu wa kutumia Silaha yamepungua kwa kiasi
kikubwa na jitihada za
kukabiliana na makosa ya usalama barabarani
zinaendelea ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo na majeruhi kwa
raia.
Tunapoelekea kipindi hiki cha
Sikukuu ya Pasaka, Jeshi la Polisi katika mikoa yote linawahakikishia
wananchi kuwa limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa sikukuu hii inasherekewa kwa
amani na utulivu na hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyofanyika
na pale vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi utaimarishwa kwenye
maeneo yote yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe, sehemu za starehe na
maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili
kuhakikisha wananchi wote wanasherekea sikukuu hiyo katika hali ya
utulivu.
Wazazi wanatakiwa kuwaangalia
watoto wao na kutowaacha kutembea peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa
karibu, pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria,
kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo ikiwemo kutoruhusu disko
toto na kujaza watu kupita kiasi.
Vilevile Jeshi la Polisi
linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara kuwa
makini na kuzingatia Sheria za Usalama barabarani hasa kwa madereva wa
magari na pikipiki kuepuka kujaza watu kupita kiasi, kubeba mishikaki,
kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Nawatakia Pasaka njema.
No comments :
Post a Comment