Thursday, March 29, 2018

DK. KIGWANGALLA APOKEA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA WANAOTAKA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA UTALII

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.

Na Hamza Temba - WMU-Dodoma
Kufuatia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kutafuta wawekezaji wa Kimataifa kwa ajili ya kuwekeza katika sekta utalii hapa nchini, Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China imejitokeza kwa lengo la kuwekeza katika utoaji wa huduma za kitalii zenye ladha na mandhari ya Kichina.

Mwenyekiti wa Kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Tony, amesema kampuni hiyo imepanga kujenga hoteli za kitalii za kichina katika mji wa Karatu jijini Arusha na Serengeti mkoani Mara.

Akizungumza na Waziri wa Maliasil na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ofisini kwake mjini hapa jana kwa ajili ya kutambulisha mradi huo, Tony alisema mradi huo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii wa China wanaotembelea Tanzania.

Alisema kupitia mradi huo jumla ya magari 500 ya safari za utalii yatanunuliwa (Safari Cars) kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii hao wakati wa kutembelea maeneo ya vivutio hapa nchini.

Pamoja na magari hayo alisema kampuni hiyo pia imepanga kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kutoka China hadi Tanzania ili kupunguza muda wa usafiri na gharama.

"Kupitia mradi huu, tunategemea kuhudumia watalii 200,000 kwa mwaka kutoka nchini China na kutengeneza ajira zaidi ya 200 kwa Watanzania" alisema Tony.

Alisema kwa sasa ni watalii 35,000 tu kutoka China wanaotembelea Tanzania kwa mwaka, na kwamba kupitia mradi huo idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema mradi huo umekuja wakati muafaka wakati huu Serikali kupitia Wizara yake imeshaweka mikakati mahususi ya kupanua wigo wa soko la utalii nchini China.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo inayolenga kuvutia watalii zaidi ya 200,000 kwa mwaka katika kipindi cha muda mfupi wa miaka mitatu, ni kuwakaribisha wachina wenyewe kuja kuwekeza kwenye mahoteli na huduma zenye ladha na mandhari ya kikwao. Mataifa mengine ni Israel, Urusi na Oman.

Alisema kwa sasa ni idadi ndogo tu ya watalii wa China wanaotembelea Tanzania ukilinganisha na ukubwa wa soko la nchi hiyo.

Aliahidi kuwapa ushirikiano wawekezaji hao ikiwa ni pamoja na kuwapa maeneo kwa ajili ujenzi wa hoteli hizo za kitalii ndani ya maeneo ya hifadhi ili kuwezesha ongezeko la watalii kutoka nchini humo.

"Kwa yale maeneo mtakayohitaji ambayo yapo nje na maeneo yetu ya hifadhi tunayoyasimamia, tutawasiliana na mamlaka husika ili muweze kuapatiwa maeneo ya kuanzisha uwekezaji huo muhimu kwa taifa" alisema Dk. Kigwangalla.

Aliwataka pia wawekezaji hao kupitia taratibu zote za kuwekeza hapa nchini ikiwa ni pamoja na kujisajili katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kusajili kampuni ya utalii hapa nchini na kuwasilisha andiko la mradi na namna ya utekelezaji wake.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza apa nchini katika ujenzi wa mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.
Wawekezaji wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing kutoka nchini China wakiwa kwenye mazungumzo na Waziri Kigwangalla ofisini kwake mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi flash yenye picha za wanyamapori wa Tanzania Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Tibet Dexin Financia Leasing, aliyefahamika kwa jina moja la Tony kutoka nchini China ofisini kwake mjini Dodoma jana wakati kampuni hiyo ilipowasilisha mpango wake wa kuwekeza hapa nchini katika ujenzi wa mahoteli na huduma za utalii zenye ladha na mandhari ya kichina.
             Waziri Kigwangalla akiendelea na mazungumzo na wakezaji hao.
SOMA ZAIDI »

No comments :

Post a Comment